Tumieni busara, ukweli na uzuri unaofumbatwa katika Injili ili kugusa akili na mioyo
ya watu wanaotafuta maana ya maisha!
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano wa SIGNIS unaofunguliwa
rasmi tarehe 25 Februari 2014 mjini Roma, ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali
Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, vyombo vya mawasiliano ya kijamii
vinachangia kujenga uzoefu, matumaini na mashaka miongoni mwa vijana wa kizazi kipya.
Huu
ni ulimwengu wa utandawazi unaofumbata tamaduni, lugha na vielelezo vipya vinavyoonesha
mwingiliano wa kijamii. Waamini wa Kanisa Katoliki wanaotekeleza dhamana na wajibu
wao katika vyombo vya Upashanaji habari wanaendelea kuchangamotishwa kutumia: busara,
ukweli na uzuri unaofumbatwa katika Injili ili kugusa akili na mioyo ya watu ambao
wana kiu ya maana ya maisha na wanataka kuwa na mwongozo kamili katika maisha yao
ndani ya Jamii.
Baba Mtakatifu anaonesha matumaini yake kwamba, mkutano huu
utawawezesha wajumbe kupata mwelekeo mpya pamoja na ujasiri wa kusonga mbele kwa imani
na matumaini ili kukabiliana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu
wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari.