2014-02-24 10:45:30

SIGNIS yaanza mkutano wake mkuu wa Mwaka 2014 mjini Roma


Zaidi ya wajumbe 300 kutoka katika nchi 80 wako mjini Roma tayari kuhudhuria Mkutano mkuu wa SIGNIS kwa mwaka 2014 unaoongozwa na kauli mbiu "Vyombo vya habari katika utamaduni wa amani: kutengeneza taswira na vijana wa kizazi kipya". Mkutano mkuu unatarajiwa kufunguliwa rasmi, Jumanne tarehe 25 Februari 2014.

Mkutano huu unahudhuriwa pia na Askofu mkuu Claudio Maria Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii anayesema kwamba, mabadiliko makubwa yanayoendelea kujitokeza katika teknolojia ya habari na mawasiliano ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi barabara, ili kuweza kuwashirikisha wengine uzuri na furaha ya Habari Njema ya Wokovu inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hii ni changamoto ya kutumia kwa ukamilifu mkubwa picha na taswira katika utekelezaji wa majukumu na dhamana ya Wakatoliki katika sekta ya mawasiliano ya Jamii.

Katika mkutano huu, Padre Gaston Roberge, SJ, Muasisi wa elimu ya vyombo vya habari nchini India pamoja na Monsinyo Roland Abou Jaoude, Muasisi wa Kituo cha Habari za Kikatoliki Lebanon watapewa tuzo maalum ya SIGNIS kwa kutambua mchango wao katika sekta ya mawasiliano ya jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.