Maaskofu wa Hispania waanza hija ya kitume mjini Vatican
Kundi la kwanza la Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania, tarehe 24 Februari 2014 linaanza
hija ya kitume inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano kadiri
ya sheria za Kanisa. Kundi la kwanza linaundwa na Maaskofu 44, litapata nafasi ya
kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu pamoja na viongozi waandamizi kutoka Vatican.
Taarifa zinaonesha
kwamba, kundi la pili litakutana na Baba Mtakatiofu Francisko kuanzia tarehe 3 hadi
tarehe 8 Machi 2014. Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na Maaskofu wote wa Hispania
hapo tarehe 3 Machi 2014. Kwa mara ya mwisho, Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania
lilifanya hija yake ya kichungaji kunako mwaka 2005. Hata kama walihitimisha hija
yao kadiri ya sheria za Kanisa, lakini hali ya Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili iliendelea
kudhohofu sana.
Katika uongozi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Baraza
la Maaskofu Katoliki Hispania halikupata nafasi ya kufanya hija ya kitume mjini Vatican.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alibahatika kutembelea Hispania mara tatu wakati
wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mara ya kwanza ilikuwa ni Mwaka 2006
wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Tano ya Familia Kimataifa iliyoadhimishwa mjini Valencia.
Kunako mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI alitembelea mjini Barcelona
na Santiago de Compostella.
Vijana wengi wanaikumbuka hija ya kichungaji ya
Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI mjini Madrid wakati wa Maadhimisho ya Siku ya
Vijana Duniani kwa Mwaka 2011, wakati vijana waliponyeeshewa na mvua kubwa na Baba
Mtakatifu mstaafu Benedikto akabaki pamoja nao! Adhimisho likaendelea kama ilivyopangwa
kwa Kesha na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu.