2014-02-24 09:34:37

Bado kuna umuhimu wa kuwafunda Waamini walei, Watawa na Makleri kuhusu Liturujia mintarafu Mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican


Kongamano la Kimataifa kuhusu Jubilee ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Waraka wa Kichungaji kuhusu Liturujia ya Kanisa, lililoandaliwa na Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano limehitimishwa hivi karibuni mjini Roma.

Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe washiriki wa Kongamano hili akionesha shukrani zake za dhati kwa changamoto na mabadiliko yaliyoibuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu utukufu wa Mungu na ujenzi wa Kanisa la Kristo, tayari kusoma alama za nyakati. Waraka wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu Liturujia umeliwezesha Kanisa kufahamu kwa kina zaidi Liturujia katika mwanga wa Ufunuo mintarafu utume wa Yesu Kristo kuhani mkuu, unaoendelezwa na Fumbo la mwili wa Kristo, yaani Kanisa.

Yesu ndiye mhusika mkuu wa kila adhimisho linalofanywa na Mama Kanisa kwa kushirikiana na Kanisa ambalo ni mchumba wake ili kumpatia Mwenyezi Mungu sifa na utukufu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu yenye mvuto kwa viumbe vyote. Adhimisho makini la Liturujia anasema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa Kongamano la Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Liturujia, kwamba ni ile hali ya mtu kujisadaka mwenyewe, kama dhabihu iliyo hai, takatifu na yenye kumpendeza Mungu.

Ni changamoto na mwaliko kwa waamini kujijimina mbele ya Mwenyezi Mungu na kumruhusu Kristo kufanya mabadiliko katika maisha ya wafuasi wake, kwa kuingia kabisa katika maisha ya Mungu. Kwa maneno mengine, Liturujia inapania kumwabudu Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa.

Baba Mtakatifu anasema, Mama Kanisa anapomshukuru Mwenyezi Mungu kwa Jubilee ya Miaka 50 ya Waraka wa Liturujia, anatoa changamoto na mwaliko kwa waamini kusonga mbele kwa imani na matumaini katika hija ile iliyoainishwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kwani bado kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kutekelezwa kadiri ya mageuzi yaliyoletwa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Hapa Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa majiundo makini kuhusu Liturujia kwa waamini walei, watawa pamoja na Makleri katika ujumla wao.







All the contents on this site are copyrighted ©.