Madai ya posho ya wabunge wa Bunge maalum la Katiba inawachefua watanzania!
TGNP Mtandao tumesikitishwa na taarifa za wajumbe wa Bunge maalum la Katiba lililoanza
Februari 18, 2014, kudai nyongeza ya posho kutoka shilingi 300,000/= hadi sh. 500,000/=
kwa siku. Sisi TGNP Mtandao kama shirika linalotetea haki na usawa wa kijinsia katika
kuhakikisha rasilimali za taifa zinawanufaisha wananchi wote hatukubaliani kwa namna
yoyote na madai hayo ya wajumbe kudai posho zaidi kwa wakati huu ambao taifa lina
uhaba mkubwa wa fedha na deni la taifa likiongezeka kwa kasi kubwa hadi kufikia trilioni
27.
Inasikitisha kuona wawakilishi tuliowatuma Dodoma kujadili rasimu ya
Katiba mpya akili na mawazo yao yote yakielekezwa katika posho. TGNP tunajiuliza
Shilingi 300,000/= kwa siku ni kidogo? Hicho kiasi ni zaidi ya mshahara wa baadhi
ya watumishi serikalini na sekta binafsi ambao wanapambana kulea familia kwa mshahara
huo huo na pindi wakidai kuongezewa maslahi yao wabunge wameshindwa kuwatetea?. Ni
wabunge hawa ambao wameshidwa kupigania haki za wanawake na wanaume wanaopata kima
cha chini cha mishahara kipandishwe. TGNP Mtandao tunapinga mpango huu wa kuongeza
posho kwasababu unajenga tabaka miongoni mwa jamii na ndani ya Bunge na kuiingizia
serikali mzigo wa gharama ambazo mwishowe atazilipa mwananchi masikini.
Pia
suala la posho tunaliona kama mbinu inayotumiwa na wanaisasa wachache wasio na uzalendo
kutaka kuvuruga mchakato wa katiba mpya kwa kuhamisha mijadala yenye tija katika kuandika
katiba mpya. Tunawataka wanasiasa kuheshimu mchakato huu ambao unatumia gharama kubwa
za walipa kodi na kuhakikisha wananchi wanapata katiba mpya inayobeba masuala na sauti
zao. Kamati iliyoundwa kufuatilia posho isipoteza muda kujadili suala hilo na kupelekea
kuongezwa kwa muda wa Bunge hili zaidi ya siku 70.
Tunatoa rai kwa wajumbe
wote wa Bunge hili kuwa makini na kauli zao na kufanya kazi waliotumwa Dodoma kwa
maslahi ya taifa na anayeona kwamba fedha hazimtoshi anapaswa kurudi nyumbani ili
kutoa nafasi kwa wazalendo wa Taifa hili kuandika katiba ya Tanzania. Aidha wanaovuruga
mchakato huu wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria kwa kuliingizia taifa hasara.