2014-02-22 11:19:14

Mababa wa Kanisa waguswa na mahangaiko ya watu kutokana na vita na madhulumu na nyanyaso za kidini!


Baraza la Makardinali katika mkutano wake wa kawaida uliokuwa chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, lilipata nafasi ya kufanya tafakari ya kina kuhusu umuhimu wa familia kadiri ya mpango wa Mungu na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu na Makardinali waliguswa pia na vita na kinzani za kijamii zinazoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kutuma ujumbe wa mshikamano na upendo kwa Maaskofu mahalia nchini Ukrain.

Mababa wa Kanisa waliwakumbuka pia watu wanaoteseka kutokana na vita pamoja na mashambulizi ya kigaidi, hali ambayo kwa sasa inaonekana kuwa ni jambo la kawaida kwa baadhi ya watu. Maeneo haya ni Nigeria, Sudani ya Kusini, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati na Syria. Akizungumzia kuhusu matukio haya, Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anabainisha kwamba, vurugu na matukio yote haya yanahatarisha amani na utulivu miongoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu pamoja na Makardinali wametolea sala kwa ajili ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia wanaoteseka na kudhulumiwa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wakristo wanaendelea kuhimizwa kuwa imara katika imani pamoja na kuwasamehe watesi na wote wanaowadhulumu, huku wakijitahidi kumuiga Yesu mwenyewe aliyethubutu kuwasamehe watesi wake kwani walikuwa hawajui wanalotenda!

Ni matumaini ya Mababa wa Kanisa kwamba, Jumuiya ya Kimataifa itaendelea kujielekeza zaidi katika kusaidia mchakato wa haki, amani, utulivu, umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kukuza na kudumisha utawala wa sheria na demokrasia ya kweli. Kinzani na migogoro mingi inayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia ina mwelekeo wa kidini, hali ambayo baadhi ya watu wanaweza kudhani kwamba, ni vita kati ya Wakristo na Waislam, na kusahau kwamba, haya ni mambo yanayojikita katika: uchu wa mali na madaraka; ukabila usiokuwa na tija wala mashiko; umaskini na hali ngumu ya maisha.

Kanisa Katoliki linalaani na kushutumu vita yoyote ile inayofanywa kwa msingi wa kidini na kwamba, litaendelea kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa kutafuta, kudumisha na kuenzi: haki, amani na upatanisho kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa linaendelea kuwahimiza waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, pamoja na kuonesha ushuhuda wa imani tendaji kwa njia ya matendo ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.