Jumuiya ya Wazazi Tanzania iwe ni mfano bora wa kuigwa katika malezi kwa vijana wa
kizazi kipya!
Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Jumuiya ya Wazazi nchini ni miongoni
mwa jumuiya inayoongoza na kusimamia masuala yote yanayohusu elimu, malezi bora kwa
vijana wa taifa letu hivyo lazima iangalie jinsi ya kuweza kujipambanua katika utekelezaji
wa Umoja wa Jumuiya yao. Ametoa kauli hiyo Jumamosi, Februari 22, 2014, wakati akifungua
rasmi semina ya siku tatu ya viongozi na watendaji wa Jumuiya ya Umoja wa Wazazi ngazi
ya Taifa, Mikoa na Wilaya Tanzania inayofanyika kwenye Ukumbi wa NEC, Mkoani Dodoma.
Akizungumza
katika ufunguzi huo, Waziri Mkuu Pinda aliwaeleza wana jumuiya hao kuangalia malengo
wanayojipangia aidha yawe ya muda mfupi au mrefu ili kuyatekeleza kwa kuzingatia yale
mambo ya msingi na yenye kipao mbele kwa wananchi. “Changamoto kubwa iliyopo mbele
yenu kama viongozi na watendaji wakuu wa Jumuiya hii ni namna ya kutimiza malengo
mliyojiwekea“.
Alisema, dhana ya Jumuiya ya Umoja wa Wazazi nchini ni kuongeza
na kuboresha masuala yote yanayohusu Sekta ya elimu hapa nchini: ‘‘Tumieni semina
hii kujipima kwamba mmefikia wapi katika utelelezaji wa malengo yenu kwa kuangalia
mapungufu na maboresho katika jumuiya yenu‘‘.
Jumuiya ya Wazazi ndio magwiji
mnaoongoza kwa kuwa na shule nyingi hapa nchini, hivyo jumuiya yenu ijipange na kusimamia
vema shule hizo ili kuwa vinara katika kuboresha masuala ya elimu hapa nchini. Akitoa
mfano, alisema: “Kwanini shule za binafsi zinakuwa zinaongoza kuliko shule zilizopo
ndani ya Jumuiya yenu, walau katika kumi bora iwepo shule moja kutoka Jumuiya ya Umoja
wa Wazazi alisema Waziri Mkuu”.
Kutokana na kauli hiyo, Waziri Mkuu aliiambia
Jumuiya hiyo kutumia dhana ya elimu kama ngao yao katika kuleta maendeleo katika Sekta
hiyo kwani Ilani ya chama cha Mapinduzi imetamka wazi kuongeza kasi ya upanuzi wa
Elimu ya Awali, Msingi na Sekondari lengo ambalo ni moja ya jukumu kuu la msingi la
Jumuiya ya Umoja wa Wazazi.
Aliendelea kusema kuwa Jumuiya ya Wazazi inajukumu
la kusimamia masuala yote yanayohusu maadili, jukumu ambalo halina tofauti sana na
jukumu la madhehebu ya dini kuzungumza bayana masuala ya malezi ya watoto na vijana
ambayo yamekuwa yakiporomoka kila kukicha, hivyo Waziri Mkuu alisema, jumuiya hii
itumia jukumu na nafasi waliyopewa kuhakikisha watoto wote walio ndani na nje ya jumuiya
wanafundishwa maadili.
Waziri Mkuu aliendelea kusema kuwa, Jumuiya ya Umoja
wa Wazazi ina majengo, viwanja na ardhi inayofaa kwa kilimo na shughuli za kiuchumi,
tumieni fursa hizi kwa kujenga vyuo, kuanzisha miradi ya maendeleo ambayo itawasaidia
katika kuongeza kipato katika jumuiya yenu.‘‘Mnachotakiwa ni kupanga bajeti zenu vizuri
na kusimaia utekelezaji pamoja kusimamia vizuri miradi na fursa zinazojitokea“
Pamoja
na hayo, Waziri Mkuu aliiomba Jumuiya ya Wazazi kujitokeza kuzungumzia masuala ya
Dawa za Kulevya kwa kusema kuwa, wako vijana ambao wametumbukia katika dimbwi la Dawa
za Kulevya ambazo pia wanahatarisha maisha yao kwa kupata UKIMWI: “Ni matumaini yangu
kwamba Jumuiya ya Umoja wa Wazazi itakuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii, kutoa
ushauri kwa vijana kuhusu athari za dawa za kulevya, UKIMWI na hata mkiweza kuanzisha
vituo vya ushauri”, alisisitiza Waziri Mkuu.
“Ili kuweza kuwa na Jumuiya ya
Wazazi imara ni dhahiri kuwa wanajumuiya wasimamie kanuni na maadili yanayoongoza
jumuiya yao kwa kuwaasa kuacha kujiingaza katika makundi yasiyokuwa na msingi hasa
kwa kutanguliza maslahi ya fedha katika kupata nafasi za uongozi katika kipindi hiki
cha kuelekea uchaguzi mkuu ambao huleta migawanyiko kati ya Viongozi na wanachama
na wapiga kura”. Mzingatie masuala yanayohusu kujenga na kukuza utekelezaji wa jumuiya
yenu ambayo itawasaidia kujenga jumuiya imara na kujenga chama imara kitakacho leta
viongozi imara”alisisitiza Waziri Mkuu.
Mapema, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja
wa Wazazi Taifa, Bw. Majura Bulembo, alisema lengo la semina hiyo ni kuwajengea uwezo
na kuwaongeza ufanisi Jumuiya ya Wazazi katika utekelezaji kazi zao na kuwasisitiza
kuhudhuria semina hiyo ipasavyo ili kuweza kukumbusha mapungufu na changamoto zinazojitokeza
katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Viongozi wamekuwa wakitumia
vibaya nafasi za uongozi walizopewa kwa kujiona wao ndio viongozi wakuu kwa kujifanyia
maamuzi yao, viongozi kama hao wataondolewa madarakani mara moja”.