2014-02-22 12:19:59

Huu ndio uhuru wa kweli!


Yesu yuko bado Mlimani na anaendelea kutoa hotuba. Baada ya kututia kizunguzungu wiki iliyopita. Leo anatupatia kingamtima (dawa ya kinga) ya kupigania uhuru wa kweli, uhuru wa wana wa Mungu. Kama wewe ni mtu wa dini ya dhati na siyo dini ya chati tu, au kama wewe ni mkristu kweli, fuatilia kidhati hotuba ya leo, itakuweka sawa. Yesu anaanza kwa kusema: “Mmesikia kwamba imenenwa: Jicho kwa jicho, na jino kwa jino,”.

Usemi huu unafahamika na kupendwa na wengi kwa vile unaonekana kutetea haki, kwa vile kuna kulipiza kisasi. TunaHivi usemi huu unajulikana na kupendwa hata na wale wasioijua biblia utawasikia wakisema: “Nimempa vidonge vyake, hawezi kunichezea mimi!” “Ni wakati wa kuacha unyonge, na uvumilivu una kikomo chake.” Amri hiyo ya jicho kwa jicho, na jino kwa jino; inamanisha kutokuwa mnyonge na kuonewa bure. Kabla ya sheria hii, kulikuwa na kulipizana kisasi cha kutisha ili kumkomesha mwovu. Mathalani, kama mtu mmoja wa kijiji amempiga askari jeshi aliyemfumania kwa mke wake, basi huyo askari aliyepigika ataenda kikosini na kukusanya askari wenzake watarudi na kupiga ovyo wanakijiji karibu wote na pengine hata kuwachomea moto nyumba zao ili kuwakomoa na kuwakomesha.

Hivi ndivyo walilipiza kisasi saba mara sabini. Kisasi na adhabu ya namna hii ni ya kinyama na anayefanya hivi anayo akili ya kiwango cha mnyama wa porini. Haya ni maisha ya wapagani wasiomjua Mungu. Katika Agano la Kale la wayahudi wanaomfuata Mungu mmoja, yakawa mabadiliko, kwamba adhabu itolewe kulingana na uhalisia wa kosa lililofanyika. Ndipo ikaja amri ya “Jicho kwa jicho, na jino kwa jino” Yaani ni hatua ya ustaarabu na ya kutumia sheria. Toka kiwango hicho cha wayahudi, sasa sikiliza vidonge vya Yesu jinsi anavyotuweka sawa: “lakini mimi nawaambia: Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.” Yesu anataka kutuambia kwamba wewe usiingie katika mkumbo huu wa bendera fuata upepo wa kufuata sheria hii.

Tabia ya matendo ya binadamu huru mwenye akili na utashi haitokani na kuathiriwa na matendo ya mwingine. Kama vile gari lisiloweza kwenda hadi liwashwe au punda asiyeweza kwenda peke yake hadi apigwe. Matendo ya binadamu hayatokani wala kuathiriwa na uovu aliotendewa, bali na msukumo huru toka ndani ya moyo. Mtu ni huru endapo anafuata msukumo wa moyo wake na msukumo wa roho yake na siyo kuathiriwa na tendo la nje na hivi kulazimika kufanya mambo kama mnyama au mashine. Baada ya kuwekwa sawa hivyo, Yesu anatupeleka kwenye viwanja vinne vya kucheza na uhuru wetu.

Uwanja wa kwanza ni ule wa kimaadili:
“Mtu akikuzaba kofi shavu la kuume, mgeuzie na la pili”. Yesu analitaja shavu la kuume. Ukweli kama mtu anayetumia mkono wa kuume, atakupiga shavu la kushoto siyo la kuume. Ili akupige shavu la kuume budi atumie upande wa nyuma wa kiganja cha mkono wake wa kulia. Kofi aina hiyo kwa lugha ya kingoni linaitwa kofi la kumakava. Lilikuwa linatumika na mabwana wa kazi au wakuu kwa watumwa wao, (mkono wenye kidole unachovaa pete ya uongozi iliyokuwa inatumika pia kama muhuri). Kofi aina hiyo wakati mwingine lilikuwa linaacha alama ya vidole kwenye shavu licha ya kwamba lilikuwa linauma sana, ni pia alama ya ugandamizaji na udhalilishaji. Wakati ule, kumpiga mtu kofi la kumakava ilikuwa ni kosa kubwa na adhabu yake ilikuwa ni kulipa faini ya mshahara wa kazi ya mwezi mmoja.

Katika mazingira kama hayo ufanyeje? Yesu anasema, usijibu mapigo kutokana na pigo ulilolipata badala yake wewe uwe huru. Usijitetee, usimtishe, mwoneshe kwamba unashindwa kabisa kujitetea. Pato la kwanza utaona kwamba adui yako atajisikia ujinga kuendelea kuwa adui yako. Hapa haimaanishi kuwa Yesu anataka utulie labda sababu ya woga, la hasha, bali anataka ufanye tendo linalolingana na mtoto wa Mungu, yaani tendo linalosukumwa na upendo. Hata kama katika maamuzi hayo adui yako ataendelea kukukandamiza zaidi, wewe endelea kuwa na msimamo wako, wa kutofanya jambo kwa msukumo wa matendo yake. Kwa sababu kulipa kisasi ni alama ya unyonge na ni upumbavu. Unyonge na upumbavu vinajionesha katika vita, madhulumu, matumizi ya nguvu, hata yawe ya serikali, ya maaskari, ya wanasiasa, ya kiuchumi, hata katika adhabu ya kifo. Hizo zote ni alama dhahiri za unyama, unyonge na upumbavu. Hapo hayuko binadamu, hakuna dini, wala hakuna ufalme wa Mungu.

Ni kuikosea haki akili ya kawaida kufikiri kwamba anayeua adhabu yake ni kuuawa. Panapotokea madhulumu, maonevu, wewe mkristu kaza kamba ya mahusiano mema, uwe wa kwanza kusamehe. Daima kumbuka kwamba, ukristu siyo dini ya watumwa, wala si ya kunyanyasika, ya kudharaulika, dini ya wanyonge, au hata dini inayokana furaha ya kuishi. La hasha, bali ni dini ya wafalme, (manabii na wakuhani), yaani ya watu walio huru kabisa, wenye uwezo wote wa kutenguana mzunguko balaa wa kulipizana kisasi. Mkristu ni Bwana mkuu, mtawala na mtekelezaji wa kile anachokiamua na kukichagua yeye mwenyewe hata mbele ya uovu. Mkristu anao uwezo mkali wa kugundua namna au njia mpya za kutenda jambo kwa njia ya upendo. Huu ndiyo uhuru wa kweli.

Uwanja wa pili ni wa uchumi:
Atakaye kukushtaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Hili ni jambo jipya kabisa katika madokezo ya kimaadili. Yaani, kutotenda jambo ambalo litaharibu jina na sifa ya mtu. Umpende hata yule ambaye amekunyima haki zako za kiuchumi. Amekunyang’anya haki yako. Mkristu asiye huru atamburuta mwenzake mahakamani sababu za kiuchumi. Huko ni kukosa uhuru. Wewe usifanye hivyo. Huu ndiyo uhuru wa kweli.


Uwanja wa tatu unahusu haki – ukandamizaji na ulazimishanaji:
Yesu anasema: “Mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.” Wakati wa Yesu kilikuwa kitu cha kawaida kulazimishwa kufanya kitu, mathalani Simoni wa Kirene alilamishwa kubeba msalaba wa Yesu. Anayekulazimisha maili moja, wewe nenda naye mbili. Yesu anaonesha kwamba usifanye kitu ili kupata matokeo mazuri, bali wewe sukumwa na upendo. Wewe usifanye jema fulani kwa ajili ya kutegemea malipo fulani. Huu ndiyo uhuru wa kweli.

Uwanja wa nne ni wa kuwezeshwa kuvunja mzunguko balaa:
“Mmesikia kwamba imenenwa: Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako.” Hadi hapa sheria inaonekana kukubalika kwa mtu wa kawaida. Adui ni mtu wa kuchukiwa na jirani ni mtu wa kupendwa. Kumbe Yesu anatupelekakwenye uhondo wa Injili. Anataka kufutilia mbali wazo zima la uadui, kwa sababu uadui unazaa uadui. Uangamizi unazaa uangamizi. Uhalifu unazaa uhalifu, ni kama mnyororo usio na mwisho. Ni mzunguko balaa. Mtu aliye huru anauvunja mzunguko huo balaa. Kwa kufanya hivyo tu ndivyo unaweza kuwa huru.

Hivi Yesu anaendelea kusema: “Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi” Nikitaka kuwa huru sina budi nijisikie kupenda huko ni kuikjamilisha mimi mwenyewe, kwa sababu kusaidia wengine hakunipunguzii kitu chochote kile, badala yake kunanigeuza na kuwa na sura na mfano wa Mungu na kufanya maisha yangu yawe bora zaidi, tajiri zaidi na ya furaha zaidi. Jema huzaa jema, kisha huwaangazia wale walio karibu na hatimaye humrudia tena yule aliyelizaa hilo tendo jema. Imani ya kikristu inaanza kwa mageuzi ya ndani ya moyo. Endapo huna amani ndani yako, hutaweza kamwe kuwapa wengine amani. Kama ndani hakuna upendo, hatutaweza kamwe kutoa upendo. Amri ya upendo ni mlango iliyofunguka kuelekea kwenye tunu za uwezo, mamlaka, na nguvu za kimungu tunazopewa. Yaani, kupenda bila masherti yoyote yale kama Mungu anavyopenda. Huu ndiyo uhuru wa kweli.

Kiini na msingi wa uhuru wa mkristo upo katika maneno ya Yesu aliyesema: “ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni;anayewaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.” Ni kama kurithishana toka kwa baba kwenda kwa mwana: yaani, urithi wa mahusiano wa thamani, wa mahaba, wa nguvu. Sisi wakristu ndiyo tumerithishwa thamani hizo. Yesu amesema kuwa ninyi ni waana: Maana yake ninyi mnaweza pia kupenda maadui, mnaweza kufanya mambo yasiyowezekana. Wafipa wanaimba “Mvua ya Mungu inawanyeshea hata wachawi”. Huu ndiyo uhuru wa Mungu. Yesu anatuambia “Mimi ninaweza kuwapa uwezo huo wa kimungu: kama mtahitaji, kama mtaniuliza, mtaniomba, kama mtaifuata ile njia ya mabadiliko toka ndani ya moyo. Kwa hiyo, mimi ninahamasika. Najua nitaweza kupenda kama anavyopenda Mungu!

Biblia nzima toka mwanzo hadi mwisho inaimba: Moyo mkuu, Mungu anatupenda, Mungu ni upendo. Moyo huo mkuu wa Mungu, ni moyo ule ambao sisi tunaweza kujiunda, ni moyo ambao tunao. Kwa sababu kila mara tunapomwomba Bwana, anipe moyo mpya, unifanye mtu mpya, tunaomba kuwa na moyo wa Mungu, kuwa na moyo huo ndani yetu na vionjo na fikra zilezile kama alizo nazo Yesu Kristu. Itakuja siku, ambapo moyo wetu uliotaabika sana katika kujifunza kupenda, utakuja kuwa moyo uleule wa Mungu, tutapenda kwa upendo ule unaodumu milele, utakuwa moyo wetu, utakuwa moyo wa ulimwengu. Huyu ndiyo Mungu, na ndiyo uhuru wa waana wa Mungu upo kama upendo wa mama: atampenda mwanae wa kuzaa siyo kutokana na malipo fulani atakayofanyiwa na mtoto. Mtoto anaweza hata kuwa mbaya kupindukia lakini mama anampenda tu.

Yesu anasema: Ninyi muwe wakamilifu kama baba yenu aliye mbinguni alivyo. Yaani wewe unayo damu ya kimungu, hivyo iache hali hiyo ijioneshe, uiishi hali hiyo katika uovu na katika wema. Huo ni wema kamili wa Mungu usio na mipaka. Hayo ndiyo matumizi bora ya uhuru wa waana wa Mungu.

Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.