2014-02-21 09:00:25

Ulevi wa kupindukia ni chanzo cha majanga mengi duniani!


Zaidi ya watu millioni mbili na nusu hufariki dunia kila mwaka kutokana na ulevi wa kupindukia. Waathirika wakubwa wa janga hili la ulevi ni vijana kuanzia miaka kumi na mitano, hali ambayo inahatarisha usalama na ustawi wa maisha ya vijana hawa kwa siku za usoni kiasi kwamba, wanaweza kukosa dira na mwelekeo wa maisha. RealAudioMP3
Inasikitisha kuona kwamba, vijana wenye umri mdogo kabisa wanaathirika kwa unywaji wa pombe kupindukia. Ulevi ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kuchangia magonjwa na vifo vya ghafla. Hii ndiyo maana wataalam wa masuala ya afya wanasema kwamba, ulevi wa kupindukia ni hatari kwa maisha ya binadamu, kwani pombe si maji wala “juice”.
Kutokana na changamoto hizi, Taasisi ya Kipapa ya Sayansi Jamii, hivi karibuni iliendesha warsha ya siku moja iliyoaunganisha wanasayansi na viongozi wa Kanisa ili kufanya tafakari ya kina kuhusu madhara ya ulevi wa kupindukia katika maisha ya vijana, jambo ambalo linapaswa kuwekewa mikakati maalum ya kichungaji, ili kuwasaidia vijana kuheshimu zawadi ya maisha yao binafsi na yale ya jirani zao.
Ulevi wa kupindukia ni tatizo linalopaswa kuvaliwa njuga kwa ajili ya ustawi na mafao ya mtu binafsi na Jumuiya kwa ujumla. Hii ndiyo kauli mbiu iliyofanyiwa kazi na wadau mbali mbali kutoka ndani na nje ya Vatican. Katika tafakari yake, Kardinali Oscar Rodriguez Maradiaga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis, amekazia umuhimu wa kupambana na ulevi wa kupindukia kwa kujikita katika kanuni maadili na utu wema.
Ulevi ni jambo linaloathiri afya ya mtu, kiasi hata cha kumong’onyoa tunu msingi za kimaadili na utu wema, Ulevi umekuwa pia ni chanzo cha ajali nyingi barabarani pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na miundo mbinu inayogharimu kiasi kikubwa cha fedha ya walipa kodi.
Takwimu zinaonesha kwamba, Bara la Ulaya linaongozwa kwa ulevi wa kupindukia. Inakadiriwa kwamba, kuna zaidi ya watu millioni kumi na tano wanaosumbuliwa na ugonjwa wa ulevi wa kupindukia. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, hali ya ulevi Barani Ulaya hakuongezeka sana, pengine hii inatokana na kampeni zilizoendeshwa na wadau mbali mbali dhidi ya ulevi wa kupindukia. Kiasi cha Euro billioni 156 zinatumika kila mwaka kwa ajili ya kugharimia hasara zinazojitokeza kutokana na ulevi wa kupindukia.
Huduma kwa watu wanaosumbuliwa na ugonjwa waulevi wa kupindukia bado ni kidogo sana, kwani baadhi ya watu wanadhani huu si ugonjwa wa kupatiwa tiba bali ni starehe. Inawezekana kabisa kwa mlevi kuachana na tabia hii akizingatia masharti pamoja na kuendelea kupokea ushauri nasaha. Inasikitisha kuona kwamba, vileo ni kati ya bidhaa zinazoyaingizia mataifa mengi fedha ya kodi ya mapato. Lakini umefika wakati wa kuangalia pia afya na usalama wa maisha ya raia kwa kuweka mikakati ya kudhibiti tabia ya ulevi wa kupindukia.








All the contents on this site are copyrighted ©.