Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya Saba ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican kipindi tafakari masomo Dominika, ninakuletea
ujumbe wa Neno la Mungu nikisema kuweni watakatifu kama Baba yenu aliye mbinguni.
Huo ndo wito wa kila awaye yote anayetaka kupata wokovu yaani uzima wa milele. Tuko
tayari Dominika ya VII ya mwaka A wa Kanisa. Katika Somo la
kwanza kutoka Kitabu cha Mambo ya Walawi, tunapata kuanza kusikia mwaliko wa kuwa
watakatifu tukifuata mfano thabiti na wa uhakika yaani Mungu mwenyewe. Mungu anawasiliana
na taifa lake kwa njia ya Musa akitaka wawe watakatifu kama yeye alivyo. Anasonga
mbele akieleza kilichomo ndani ya safari ya utakatifu: kuachana na chuki, kukemea
maovu yanayojiri katika jumuiya na majirani zetu na kuachana na kinyongo na kisirani
katika maisha yako. Ili kutekeleza haya lazima kujitenga na dunia, kama iliyo maana
ya utakatifu katika Agano la Kale (mkumbuke Mtakatifu Antonio Abate, mwanzilishi wa
Umonaki).
Kwa hakika utakatifu ulikuwa na maana ya kuwekwa pembeni kwa ajili
ya Mungu. Patakatifu pa patakatifu palimaanisha Mungu mwenyewe. Ni katika maana ileile,
wakristu lazima wajitenga kiroho na chachu ya dunia yaani kuachana na maisha ya dhambi.
Ndiyo kusema kukazia amri ya mapendo kwa jirani na si kujitenga na wapagani kama Waisraeli
walivyokuwa wakifikiri. Ni kumpenda Mungu tukiambatana na wenye shida mbalimbali tukielekea
wote mbinguni.
Mtume Paulo anapowaandikia Wakorinto anakazia ule utakatifu
tuliokabidhiwa na Mungu. Anasema sisi ni hekalu la Roho Mtakatifu. Mpendwa msikilizaji,
nikishasikia neno hilo mara moja mwaliko ni kutunza utakatifu ili niendelee kubaki
Hekalu safi kwa ajili ya kumwabudia Mungu. Katika Ukorinto kulikuwa na ugomvi na ulitokana
na tishio la kutopendana na hapa ndipo Mtume Paulo anakuja na fundisho kali akikemea
uozo huo unaojitokeza katika sura ya utengano.
Katika Injili, Mwinjili Matayo,
anaweka mbele yetu mausia ya Bwana kuhusu sheria ya kale. Bwana anataka mabadiliko
ya uelewa wa sheria, yakwamba ni kwa ajili ya kujenga umoja kwa watu na si kuangamiza.
Anataka sheria izame katika utu zaidi kuliko mambo mengine na ilinde maisha, iliyo
zawadi ya Mungu. Mpendwa mwanatafakari, Hata hivyo yatupasa kuelewa nini maana ya
sheria za zamani, mfano Jicho kwa jicho au jino kwa jino!! Mara kadhaa tunatafsiri
jambo hili kadiri ya maneno yalivyo kwa nje! Na hivi huleta maana potofu! Kwa hakika
mwanzo wa sheria hii ulikuwa mzuri!
Maana yake nini! Ni kwamba kabla ya sheria
hii mtu alipokuwa akitenda kosa fulani alikuwa analazimika kulipa fidia si kwa makosa
yake tu bali hata kwa makosa mengine yasiyo yake. Na hivi ikawa ni mateso makubwa
kwa watu, basi ikatungwa sheria ya jicho kwa jicho, yaani mtu alipie fidia ya makosa
yake tu! Kumbe kukazaliwa namna mpya na ya haki katika kutawala na kuongoza haki katika
JUMUIYA. Ndiyo kusema hakukuwa na matumizi ya moja kwa moja yaani ya kuondoana macho
au meno! Ndiyo kusema walitaka kufundisha ule uwiano kati ya kosa na adhabu .
Mpendwa
msikilizaji, Bwana anasema imeandikwa jicho kwa jicho kama njia ya kutenda, lakini
mimi nasema epukeni magomvi, majibizano katika maisha yenu. Ni heri kuvumilia na kuachana
na mwendelezo wa mapigano. Hataki kuondoa haki ila anataka kuwepo na upole na unyenyekevu
wa moyo katika maisha ya watu wakitafuta haki, ili mbele ya taabu tupate kutunza umoja
na utulivu katika jumuiya.
Bwana anafundisha kwa hakika, njia ya pekee ya kuondoa
mnyololo wa fitina ni msamaha. Kwa maana mtu akikupiga na ukamsamehe mara moja hakuna
nyongeza ya ukubwa wa mapigano, lakini kama ukijibu kwa mapigano basi nyongeza mara
mbili ya shida katika jumuiya. Anazidi kukazia upendo hata kwa adui, na hii ndiyo
namna ya kwenda kinyume na mantiki ya zamani kuhusu upendo.
Mpendwa, mantiki
ya zamani na ya sasa kuhusu upendo ni ipi? Kwa hakika hapo zamani ilikuwa mpende akupendaye
kinyume na mantiki ya Kristu katika Agano Jipya isemayo, mpende hata adui yako. Bwana
haondoi ile ya kwanza bali anaiongezea nguvu na kuikamilisha. Mpendwa, yashike haya
yote yaliyousiwa na Bwana na kuyaishi na hivi utakuwa mtakatifu kama Baba yetu aliye
mbinguni.
Nikutakie furaha na matumaini katika kuishi sheria mpya, sheria ya
Mungu itujengeayo uhuru na mshikamano na Kristo. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.