Salini kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro wakati wa Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu
Petro
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 22 Februari 2014 katika Maadhimisho ya Siku
kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, anatarajiwa kuongoza Ibada ya Neno la Mungu kwa kuwasimika
Makardinali wapya 19 aliowateuwa hivi karibuni kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Ni tukio ambalo litakuwa na sehemu kuu tatu: sehemu ya kwanza: Makardinali
wapya watapewa kofia nyekundu za Ukardinali; pili watapewa pete ya Ukardinali na tatu,
watakabidhiwa Makanisa ya huduma mjini Roma kwani kwa kutangazwa kuwa Makardinali
wanakuwa ni wasaidizi na washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.
Ibada
itakayotumika Jumamosi wakati wa kuwasimika Makardinali ni ile ambayo imefanyiwa Marekebisho
makubwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita. Ikumbukwe kwamba, Ukardinali
si Sakramenti bali ni heshima ambayo Kanisa linawatunukiwa baadhi ya watoto wake kwa
ajili ya kusaidia mchakato wa kuliongoza Kanisa la Kristo. Kardinali mteule Pietro
Parolin ndiye atakayetoa neno la shukrani kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya
Makardinali wenzake wote, siku ya Jumamosi.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili
ijayo tarehe 23 Februari 2014 ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro akiwa amezungukwa na Makardinali wapya.
Baba Mtakatifu
Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kusali kwa ajili
ya kumwombea ili aweze kutekeleza vyema dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu
Petro; tayari kushuhudia kwa njia ya imani tendaji ujenzi wa Kanisa la Kristo.