Mambo msingi yanayogusa utu na heshima ya binadamu!
Zawadi ya uhai, tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; uhuru, dhamana na wajibu
wa wazazi na walezi katika majiundo makini ya watoto wao pamoja na umuhimu wa kusimama
kidete kulinda na kudumisha mafao ya wengi ni kati ya mambo makuu yaliyojitokeza kwenye
ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia katika Maadhimisho ya Siku ya Uhai Kitaifa,
iliyoadhimishwa, hivi karibuni. Haya ni mambo msingi yanayogusa utu na heshima ya
mwanadamu bila kusahau mchango wa Kanisa katika sekta ya elimu. Waamini na watu
wenye mapenzi mema nchini Italia wanaendelea kuhamasishwa kusimama kidete kulinda
na kutetea Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; uhuru usiokuwa na mipaka wala
kuzingatia maadili na utu wema. Sheria zinazotaka kufuta tofauti msingi za kijinsia
kwa ajili ya kulinda uhuru wa baadhi ya wananchi ni kuhatarisha maana, dhamana na
mchango wa maisha ya ndoa na familia. Matumizi ya maneno “Baba” na “Mama” bado
ni muhimu sana katika kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kumbe, kuna
haja kwa wanasiasa kuwa makini katika mikakati ya majiundo ya vijana wa kizazi kipya,
kwa kukuza na kuunda dhamiri nyofu, ili kutoa nafasi kwa vijana kutambua mema ya kufuata
na mabaya ambayo wanapaswa kuepukana nayo. Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba, wanasiasa
wanakimbilia kutunga sheria zinazohatarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia
wanasema Maaskofu Katoliki Italia. Jamii inapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza
kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Kila mwanadamu
anapaswa kulindwa na kuheshimiwa, lakini zaidi kwa wale wasiokuwa na sauti, kwa kuondokana
na sera za ubaguzi, nyanyaso na madhulumu kwa wanawake. Maaskofu wa Italia wanasema,
Ndoa kati ya Bwana na Bibi ni matunda ya upendo wa dhati kati ya mume na mke, wanaotambua
kwamba, wanashirikishwa kwa namna ya pekee katika kazi ya Uumbaji na malezi ya watoto
wao. Kimsingi wazazi ni walinzi wa zawadi ya maisha, tunu msingi za maisha ya
ndoa na familia pamoja na elimu makini kwa watoto wao. Kamwe wanasiasa wasitake kuwavuruga
wananchi kwa kuanzisha dhana na mambo ambayo hayana mafao wala mashiko kwa mtu binafsi
na Jamii kwa ujumla. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaangalisha kwamba, haiwezekani
kuanzisha siasa za usawa wa kijinsia inayosigana na ukweli msingi wa tofauti zilizopo
kati ya mwanaume na mwanamke, kiasi cha kulinda mwelekeo huu potofu kwa njia ya sheria.
Maaskofu wanapenda bado kusikia watu wakitumia maneno “mke wangu”, “Baba”, “Mama”
au “Mume wangu”; dhana inayofumbatwa katika maisha ya ndoa na familia kati ya mume
na mke. Huu ndio utashi wa Mungu katika maisha ya binadamu katika mchakato wa kumshirikisha
katika kazi ya Uumbaji. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linaendelea kuwatia
shime waamini na watu wenye mapenzi mema wanaotekeleza wajibu wao katika mazingira
na changamoto kubwa kama hizi, kutoka tamaa bali kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu,
huku wakishuhudia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; tofauti za kijinsia kati
ya mume na mke; uhuru wa kidini na umuhimu wa wazazi na walezi katika kushiriki kikamilifu
katika mchakato wa elimu na majiundo makini ya watoto wao: kiroho na kimwili. Kanisa
daima linapenda kulinda na kutetea mafao ya wengi ndani ya Jamii. Zawadi ya uhai katika
hatua zake msingi ni mambo yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Kanisa, kwani linatambua
kwamba, uhai ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Maaskofu wanapenda kuonesha
mshikamano wao wa dhati na wananchi wote wa Italia wanakabiliana na athari za myumbo
wa uchumi kimataifa. Wanawasihi kwamba, licha ya magumu na changamoto mbali mbali
za maisha, waendelee kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya Uhai.