Jitokezeni kushiriki kwenye uchaguzi mkuu hapo tarehe 7 Mei 2014
Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linawahamasisha waamini na wananchi wote
wa Afrika ya Kusini katika ujumla wao kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika
kupiga kura hapo tarehe 7 Mei 2014. Hii ni haki ambayo wananchi wa Afrika ya Kusini
wameipata baada ya watu wengi kumwaga damu yao ambayo imekuwa ni mbegu ya demokrasia
katika kipindi cha miaka ishirini tangu utawala wa ubaguzi wa rangi ulipoondolewa
nchini Afrika ya Kusini.
Huu utakuwa ni uchaguzi mkuu wa tano kufanyika nchini
Afrika ya Kusini baada ya kuanguka kwa utawala wa ubaguzi wa rangi. Wananchi wa Afrika
ya Kusini wanaweza kuamua kufanya mageuzi kwa njia ya kura zao. Afrika ya Kusini bado
inaendelea kukabiliana na cheche za ubaguzi, umaskini wa hali na kipato, ukosefu wa
fursa za ajira, miundo mbinu mibovu, huduma hafifu za kijamii, uhalifu pamoja na kudorora
kwa elimu inayotolewa nchini Afrika ya Kusini.
Licha ya mapungufu haya yaliyojitokeza
katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita, lakini Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika
ya Kusini linasema kwamba, kumekuwepo pia na mafanikio ya kuridhisha katika maboresho
ya makazi ya watu, huduma bora ya maji safi na salama kwa idadi kubwa ya wananchi
wa Afrika ya Kusini; ujenzi wa miundo mbinu ya barabara na maboresho katika huduma
za afya.
Haya ni matunda ya mchakato wa kidemokrasia yaliyofikiwa na wananchi
wa Afrika ya Kusini. Ndiyo maana Maaskofu wanawahimiza wananchi wa Afrika ya Kusini
kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu nchini Afrika ya Kusini.