2014-02-19 08:55:14

Mikakati ya Uinjilishaji wa kina Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania


Utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa maneno na vitendo, hufungua mioyo ya watu hadi kutamani utakatifu, kwa kufananishwa na Kristo na kwamba, kuhubiri Injili kunapania kwa namna ya pekee, ujenzi wa Kanisa la Kristo, changamoto inayohitaji waamini kubadilika: kiakili na kitabia, kwa kuonesha ushuhuda wa imani tendaji, maisha yanayoongozwa na nguvu ya Sakramenti za Kanisa na Liturujia ya Kanisa, Neno la Mungu na matendo ya huruma. RealAudioMP3

Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili katika Waraka wake wa kichungaji Kanisa Barani Afrika anasema kwamba, uenezaji wa Injili unahitaji mabalozi wema na watakatifu. Zaidi sana hii ni shughuli ya Kanisa la nyumbani chini ya Askofu mahalia ambaye anajukumu la kuunganisha majitoleo ya watu wa Mungu, kwa kuwathibitisha katika imani, kwa njia ya Mapadre na Makatekista ili waweze kutekeleza wajibu wao barabara.

Ili kufanikisha mikakati hii, Jimbo linahitaji kubuni mbinu mkakati wa kukusanya, kujadiliana, kupanga na kutekeleza shughuli za Uinjilishaji Mpya. Karama na vipaji ambavyo wadau wa Uinjilishaji wamekirimiwa na Roho Mtakatifu zinapaswa kutumiwa kikamilifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Ujumbe wake wa Dhamana ya Afrika anaialika Familia ya Mungu Barani Afrika kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa, kwa kuishi katika uaminifu kamili kwa Yesu Kristo na umoja katika utofauti.

Kutokana na changamoto zote hizi, Jimbo Katoliki la Ifakara ambalo linaongozwa na Askofu Salutaris Libena, lilifanya warsha ya siku nne kwa ajili ya kunoa Mihimili ya Uinjilishaji Jimboni Ifakara. Ni Warsha iliyoandaliwa na Idara ya Upashanaji habari ambayo inasimamiwa na Padre Wenceslaus Kayera, ambaye pia ni Katibu mkuu wa Jimbo Katoliki la Ifakara. Warsha hii iliishirikisha Familia ya Mungu, Jimbo Katoliki la Ifakara, ili kupanga mikakati kwa ajili ya kubainisha Mpango wa Miaka mitatu ya Shughuli za Mawasiliano, Jimbo Katoliki Ifakara.

Askofu Libena katika hotuba yake ya ufunguzi alibainisha kwamba, warsha hii ni sehemu ya mikakati ya Jimbo Katoliki la Ifakara kutaka kuainisha mipango ya kichungaji kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa Jimbo Katoliki Ifakara. Anasema, Kanisa linatambua umuhimu wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa kimsingi linatumwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano katika mchakato wa utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa.

Ili kufanikisha changamoto hii, kuna haja kwanza kwa Kanisa lenyewe kujiiinjilisha na kujitakatifuza, ili liweze kuleta mguso na mashiko kwa Watu wa Mataifa. Waamini wanaalikwa kuwaonjesha jirani zao ile Injili ya Furaha baada ya kukutana na Yesu Kristo katika: Neno, Liturujia, Sakramenti, Maskini na wote wanaosukimizwa pembezoni mwa Jamii. Huu ndio ukweli unaojipambanua ndani ya Kanisa kwa kuonesha umuhimu wa mawasiliano katika maisha na utume wa Kanisa. Hili ni jukumu linalogusa nyanja mbali mbali za maisha ya mwanadamu, mazingira pamoja na matumizi makini ya njia za mawasiliano ya kijamii.

Padre Chrisantus Ndaga, Katibu wa Idara ya Mawasiliano ya Jamii, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA, ndiye aliyekuwa muwezeshaji mkuu katika warsha hii. Anasema, washiriki walichagia sana kuweka msingi wa mikakati ya mawasiliano ya kijamii Jimbo Katoliki Ifakara katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Mihimili ya Uinjilishaji Jimboni Ifakara, ilifafanuliwa umuhimu wa mawasiliano ya kijamii, vipaumbele na dhamana yake katika mchakato mzima wa Uinjilishaji Mpya na hatimaye, wakaweka mikakati ya kichungaji katika Idara ya Mawasiliano ya Jamii kwa kipindi cha Miaka mitatu, ijayo.

Itakumbukwa kwamba, Jimbo Katoliki la Ifakara ni kati ya Majimbo machanga sana nchini Tanzania, lililoundwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 14 Januari 2012 kwa kulimega Jimbo Katoliki la Mahenge na kumtangaza Askofu Salutaris Melchior Libena kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Ifakara.








All the contents on this site are copyrighted ©.