Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameridhia kuchapwa kwa nyaraka mbali mbali
zinazowahusu watumishi wa Mungu na wenyeheri katika mchakato wa kutangazwa kuwa watakatifu
kama zilivyowasilishwa kwake na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa
la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu. Kati yao kuna:
Mtumishi wa
Mungu Padre Piet Asua Mendia, kutoka Hispania, aliyezaliwa tarehe 30 Agosti 1890 na
kuuwawa kutokana na chuki za kidini tarehe 29 Agosti 1936.
Mtumishi wa Mungu
Padre Giuseppe Girelli kutoka Jimbo la Verona, Italia, aliyezaliwa tarehe 10 Januari
1886 na kufariki dunia Mei Mosi 1978 kutokana na ushupavu wake wa kiimani.
Kanisa
limetambua karama ya ushupavu wa kiimani ulioneshwa na Mtumishi wa Mungu Padre Zaccaria
di Santa Teresa wa Shirika la Wakrameli, aliyezaliwa kunako tarehe 5 Novemba 1887
na kufariki dunia tarehe 23 Mei 1957, akiwa nchini India.
Mama Kanisa ametambua
ushupavu wa kiimani ulioshuhudiwa na Mtumishi wa Mungu Marcella Mallet, Mwanzilishi
wa Shirika la Masista wa Upendo, Quebec, aliyezaliwa tarehe 26 Machi 1805 na kufariki
dunia hapo tarehe 9 Aprili 1871.
Wengine katika orodha hii ni pamoja na Mtumishi
wa Mungu Maria Benadetta Aria, Mwanzilishi wa Shirika la Masista wahudumu wa Yesu
katika Sakramenti, aliyezaliwa tarehe 3 Aprili 1822 huko Buenos Aires, Argentina na
kufariki dunia tarehe 25 Septemba 1894 kutoka na ushupavu wake wa kiimani.
Kanisa
linatambua ushupavu wa kiimani uliojidhihirisha katika maisha ya Mtumishi wa Mungu
Margharita wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, Mwanzilishi wa Shirika la Masista Wafranciskani
wa Moyo Mtakatifu wa Yesu, aliyezaliwa kunako tarehe 28 Novemba 1862 huko Malta na
kufariki dunia tarehe 22 Januari 1952.
Mama Kanisa anatambua fadhila za ushupavu
wa kiimani zilizooneshwa kwa namna ya pekee katika maisha ya Mtumishi wa Mungu Serafina
wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu, aliyezaliwa tarehe 31 Januari
1913 na kufariki dunia hapo tarehe 21 Oktoba 1988 huko Manaus, Brazil.
Mwishoni,
Kanisa limetambua pia fadhila za kiimani zilizojitokeza katika maisha ya Mtumishi
wa Mungu Elizabeth Sanna, mjane na mwamini mlei, aliyejifunga kwa nadhiri katika Utawa
wa watu wa Mtakatifu Francisko katika huduma ya upendo na mshikamano ulioanzishwa
na Mtakatifu Vinzent wa Paolo. Yeye alizaliwa tarehe 23 Aprili 1788 Sassari, Italia
na kufariki dunia tarehe 17 Februari 1857 mjini Roma.