Mshikamano wa biashara miongoni mwa wanawake wa Eneo la Maziwa Makuu
Jimbo Katoliki la Kyangugu, lililoko nchini Rwanda hivi karibuni lilizindua mfumo
wa biashara unaopania kujenga na kudumisha mshikamano wa amani nchini Rwanda, kwa
kuwajengea wanawake uwezo katika masuala ya kiuchumi.
Mradi utawashirikisha
pia wanawake kutoka eneo la Maziwa Makuu kwani hawa ndio waathirika wa vita na kinzani
za kijamii zinapojitokeza katika nchi zao. Burundi na DRC ni kati ya nchi zitakazohusishwa
kwenye mradi huu unaotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka miwili.
Baraza
la Maaskofu Katoliki Rwanda linasema kwamba, jumla ya wanawake sitini kutoka katika
Majimbo kadhaa ya Kanisa Katoliki Eneo la Maziwa Makuu watahusishwa katika biashara
ya mshikamano kwa kubadilishana biadhaa kama njia ya ujenzi wa umoja, upendo na mshikamano
kati ya watu. Askofu Jean Damascene Bimenyimana wa Jimbo Katoliki Kyangugu, Rwanda
anasema, mradi wa Cosopax ni chombo cha kukuzia umoja, urafiki na mshikamano miongoni
mwa wanawake wa eneo la Maziwa Makuu.
Hizi ni juhudi zinazochangiwa na Jumuiya
ya Kimataifa kwa njia ya mshikamano wa kidiplomasia pamoja na wanasiasa kutoka Eneo
la Maziwa Makuu. Tume ya haki na amani, Jimbo Katoliki la Kyangungu ndiyo iliyopewa
dhamana ya kufuatilia utekelezaji wa mradi huu miongoni mwa wanawake.
Ni mradi
unaojikita katika umoja, upendo, haki na mshikamano wa dhati kati ya wanawake ambao
kimsingi ni wajenzi wa amani na uvumilivu. Wanawake wakiwezeshwa kiuchumi na kielimu
wanaweza kufanya makubwa zaidi katika Jamii zao.