Mpendwa Msikilizaji wa Radio Vatican endelea kutega sikio tuhekimishane kuhusu yale
yahusuyo maisha ya ndoa na familia. Kwa vipindi kama hivi, Kanisa linaendelea kutekeleza
wajibu wake wa kuwafundisha, kuwaombea na kuwasaidia wote walioitikia wito wa ndoa
ili waweze kutekeleza vema malengo ya wito huo.
Katika kipindi
hiki, tushirikishane juu ya vizuizi vya ndoa kadiri ya sheria ya Kanisa. Mpendwa
msikilizaji, ili somo letu lisiwe zito masikioni, tutaichambua mada hii kwa mtazamo
wa kichungaji zaidi. Tunaiweka kwa ufupi sana na kwa mifano myepesi. Undani wake mwaweza
kupata katika semina za ndoa. Kwa yale ambayo hayataweza kufafanulika vizuri hadharani
hapa, tunawaalikeni nyote waendeeni Maparoko na Mapadre wetu, waulizeni nao watawahekimisha.
Mpendwa
msikilizaji, kwa wale wenye kufuatilia mada hii katika Ngombo la Sheria za Kanisa,
tafakari hii ina uhalali kwa nguvu sheria ya Kanisa, Kanuni namba 1083 – 1094. Hapo
tunakuta vizuizi KUMI NA VIWILI. Kuna vizuizi ambavyo ni vya hadhara na vingine sio
vya hadhara. Vipo vya kijamii na vingine ni vya kiroho. Kwaye anayetaka kuingia katika
wito huo wa ndoa, kisha jua kwamba ana kizuizi, basi kitatuliwe kwa taratibu zinazokubalika.
Tunaposikia tangazo “UNGA NA MAJI WANATAKA KUFUNGA NDOA, TANGAZO LA KWANZA.
Wanaojua kizuizi chochote wapashe habari katika ofisi ya Paroko, haya yafuatayo ndiyo
ya kupeleka. Usipeleke habari isiyohusika, eti aah binti yule anakiburi huwa hanisalimii.
Au aah yule bwana anajiona sana, mimi naona hata ndoa hiyo asifunge!! Wee, hivyo sio
kizuizi kisheria. VIZUIZI VYENYEWE NI HIVI HAPA:-
Kizuizi cha kwanza ni UMRI.
Sheria Kan, namb. 1083 inaelekeza kwamba, mwanaume anaweza kuoa akiwa na umri wa miaka
16, na binti anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14. Kanisa linaona umri huo kwa
tamaduni nyingi, mtu anaweza kuchukua majukumu ya ndoa na kuhimili mikikimikiki ya
ndoa na familia. Endapo wanandoa wana umri mdogo zaidi, kizuizi kipelekwe kwa Paroko.
Hapa Kanisa limetamka tu umri wa chini. Kuhusu umri wa juu halijasema kitu na hicho
sio kizuizi (Ila hali halisi itazamwe). Mtu asiseme, aah mbona mchumba mwenyewe amemzidi
umri, au mbona wamepishana sana umri hawezi kumuoa. Hapana, wasiwe chini ya 16 na
14. Huko kwingine sio kizuizi.
Kizuizi cha pili ni UHANITHI. Sheria Kan, namb.
1084 inazingatia lengo la ndoa ‘kuzaa watoto’. Endapo mmoja hana uwezo wa tendo la
ndoa (aweza kuwa mke au mume), huyo anazuiwa kwa sheria ya asili. Hiki ni kizuizi
cha ndani, hakionekani usoni. Ni juu ya mtu binafsi kujijua.
Tutofautishe
hapa kati ya kukosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa na kukosa uwezo wa kuzaa (utasa
na ugumba). Utasa na ugumba, havizuii wala kutengua ndoa. Siku zetu hizi mang’amuzi
ya kichungaji yanashuhudia kukithiri kwa tatizo la uhanithi kwa vijana wengi wa kike
na wa kiume. Siku nyingine tutachambua sababu ya mkasa huu. Ukitambua kama fulani
ana shida hii, basi hicho ni kizuizi, asiingie kwenye ndoa atatesa mwenzake. Lakini
nyakati zetu sayansi ya tiba imekuwa sana ni vema watu kushughulikia afya zao mapema
kama kuna matatizo.
Kizuizi cha tatu ni NDOA-AWALI. Sheria Kan, namb. 1085
inakataza mtu kuoa au kuolewa wakati alikwisha kufunga ndoa na ndoa ya kwanza bado
ipo hai. Sasa, huweza kutokea mazingira kwamba wanandoa wametengana kwa taratibu za
talaka za kiserikali. Kanisa bado linatambua na kuheshimu ile sakramenti; hivyo haliruhusu
ndoa nyingine!
Changamoto ya nyakati zetu hizi, ambapo wadanganyifu ni wengi,
mtu anafunga ndoa kona mmoja ya nchi, anamtoroka mwezi wake, anakwenda kona nyingine
ya dunia anaoa au kuolewa huko wakati alikotoka ameacha mke au mume na watoto. Hilo
agano la pili ni batili. Ukisikia ndoa inatangazwa ya mtu ambaye unajua aliwahi kuoa
au kuolewa na mwenziwe yupo, kimbia kaseme, ni kizuizi hicho.
Kizuizi cha nne
ni UTOFAUTI WA IMANI. Sheria Kan, namb. 1086, inaelekeza kwamba, iwapo mmoja ni Mwamini
Mbatizwa Mkatoliki na mwingine sio, utofauti huo ni vema utatuliwe kwanza kadiri ya
taratibu zetu. (Utofauti unaoelezwa hapa ni ule kati ya Mkatoliki na Mkristo asiye
mkatoliki, au Mkatoliki na mwamimi wa dini nyinginezo). Taratibu msingi zifuatwe
ili kweli iwe Sakramenti. Baba Paroko anajua cha kufanya.
Hadi hapa ndugu mzikilizaji
wa Radio Vatican, tunaahirisha makala yetu kwa leo, Juma lijalo tutaendelea kuhekimishana
kuhusu vizuizi vya ndoa ya Kikristo kwa kuangalia kuhusu maisha ya Daraja Takatifu,
Utawa pamoja mtu kutoroshwa. Hadi wakati mwingine tena ni mimi Padre Pambo Martin
Mkorwe, OSB.