Katika Maadhimisho ya Siku ya wapendanao kama njia ya kumuenzi Mtakatifu Valentino,
Askofu na msimamizi wa wapendanao, aliyefariki dunia hapo tarehe 14 Februari mjini
Roma kunako karne ya nne, wanandoa watarajiwa thelathini elfu walimiminika kwenye
Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ili kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko.
Mkutano
wa wapendanao ni sehemu ya maandalizi ya Sinodi maalum ya Maaskofu Katoliki kuhusu
Familia itakayofanyika mwezi oktoba hapa mjini Vatican. Wanandoa watarajiwa walipenda
kukutana na kusali pamoja na Baba Mtakatifu Francisko aweze kubariki upendo wao, ili
siku watakapofunga Sakramenti ya Ndoa, upendo wao udumu hadi watu washangae!
Hili
ni kundi la Waamini linalotaka kuendeleza kazi ya uumbaji na malezi kwa watoto ambayo
Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu katika hija yake ya maisha ya hapa duniani, kwa
kumuumba mwanaume na mwanamke ili waweze kutegemezana. Ni kundi linalotaka kujenga
na kuimarisha misingi ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu na wala si katika hali ya
kujisikia na vionjo vya kibinadamu, mambo ambayo kimsingi ni mambo mpito!
Ni
sehemu ya hotuba iliyotolewa na Askofu mkuu Vincenzo Paglia, Mwenyekiti wa Baraza
la Kipapa la Familia wakati alipokuwa anamkaribisha Baba Mtakatifu Francisko ili aweze
kujibu maswali na duku duku za wanandoa watarajiwa waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja
wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Kanisa limewakumbuka wanandoa watarajiwa
pamoja na watoto wanaokumbana na nyanyaso, vitisho na dhuluma, kwani haya ni mambo
ambayo kamwe hayawezi kukubalika yaendelee bila kushughulikiwa kikamilifu.
Askofu
mkuu Vincenzo Paglia anasema, wanandoa watarajiwa wametoka katika nchi thelathini,
ongezeko kubwa kupita hata yale matarajio na idadi iliyokuwa imetolewa na Baraza la
Kipapa la Familia siku chache zilizopita. Wanandoa hawa wanapenda kwa pamoja katika
maisha ya ndoa na familia waweze kushirikiana ili kukabiliana na changamoto zinazojitokeza
katika maisha.
Ni dhamana na jukumu la wanasiasa na watunga sera kuhakikisha
kwamba, wanazisaidia familia kutekeleza dhamana na wajibu wake katika Jamii na Kanisa
kwa ujumla. Kwa vijana wanaothubutu kujenga na kuimarisha msingi bora wa maisha ya
kifamilia tangu ujana wao, hawa wanakuwa ni utajiri mkubwa kwa Jamii husika! Wanandoa
watarajiwa wamekumbushwa kumualika Yesu katika maisha ya ndoa yao!
Baba Mtakatifu
Francisko akijibu maswali ya wanandoa watarajiwa amewataka wajikite katika upendo
dumifu hadi kifo kitakapowatenganisha na hivyo kukataa katu katu upendo mpito! Amewataka
wajitahidi kumwilisha ndani mwao tunu msingi za maisha na mtindo wa ndoa ya Kikristo:
kwa kuombana na kusameheana; kwa kushukuru! Haya ni mambo msingi yanayorutubisha udumifu
wa maisha ya ndoa na familia.
Baba Mtakatifu amewataka wanandoa watarajiwa
kuzingatia mambo msingi katika maadhimisho ya Sakramenti ya Ndoa, ili kuweza kufurahia
siku hii muhimu katika maisha yao!