2014-02-15 15:28:19

Uhuru wa kidini ni msingi wa haki zote za binadamu!


Uhuru wa kidini ni kati ya haki msingi za binadamu zinazopaswa kulindwa na kuendelezwa kwa kuheshimu na kuthamini dhamiri ya mtu binafsi na Jamii katika ujumla wake. Hii ni haki inayojikita katika masuala ya kidini na uhuru wa kuabudu. Uhuru wa kidini unapata chimbuko lake katika utu na heshima ya binadamu.

Lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, madhulumu na nyanyaso za kidini dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia yanazidi kuongezeka mwaka hadi mwaka hata katika nchi zile ambazo zinadai kwamba, zinafuata demokrasia, hali inayoonesha kinzani katika uelewa na ufahamu wa demokrasia ya kweli!

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Francis Chullikatt, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati alipokuwa anachangia mada kuhusu uhuru wa kidini kwenye Ikulu ya Marekani, huko Washington DC. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, aliwahi kusema kwamba, ukosefu wa uhuru wa kidini sehemu mbali mbali za dunia, unatishia amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa. Uhuru wa kidini ni kati ya mambo msingi yanayopaswa kusimamiwa kikamilifu na Umoja wa Mataifa kwani ndiye mhusika mkuu.

Serikali ya Marekani ni mdau na mshawishi mkuu katika masuala ya utekelezaji wa uhuru wa kidini sehemu mbali mbali za dunia, kumbe, Serikali ya Marekani inapaswa kutekeleza dhamana hii kwa kutumia ushawishi wake katika Jumuiya ya Kimataifa. Uhuru wa kidini Mashariki ya Kati uko mashakani na hapa bado kuna Wakristo wengi wanaoendelea kunyanyasika kutokana na imani yao, jambo ambalo haliwezi kukubalika tena! Kuna haja kwa watu kujenga na kuimarisha amani na utulivu kwa kuheshimiana katika tofauti zao za kidini.

Vatican kwa upande wake, itaendelea kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea uhuru wa kidini pamoja na kuzuia nyanyaso na ubaguzi wa kidini unaoendelea bado kusikika sehemu mbali mbali za dunia. Uhuru wa kidini ukiheshimiwa, amani na utulivu vinaweza kutawala tena katika uso wa dunia, kila mtu akitekeleza wajibu wake barabara, uhuru wa kidini unawezekana.







All the contents on this site are copyrighted ©.