2014-02-15 15:03:56

Msiige, mtapotoka na kukengeuka!


Shutuma zinazotolewa na baadhi ya wanaharakati dhidi ya Kanisa katoliki kuhusiana na tunu msingi za kiutu na kimaadili katika masuala kama vile utoaji mimba, vizuia mimba, matumizi ya viini tete katika majaribio ya kisayansi ni kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kimsingi, Kanisa linajipambanua katika Mafundisho yake kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; haki na amani pamoja na mafao ya wengi. Kanisa linapenda kusimamia haki msingi za binadamu. Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Ignatius Kaigama wa Jimbo kuu la Jos, Nigeria wakati wa semina maalum kwa wafanyakazi katika sekta ya afya nchini Nigeria. Semina hii ilikuwa inaongozwa na kauli mbiu "Huduma ya afya mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa"

Mafundisho Tanzu ya Kanisa yanapata chimbuko lake katika Biblia na Mapokeo ya Kanisa na hayawezi kubadilishwa kwa kushinikizwa na Serikali, wanaharakati au watu ambao wameshindwa kuheshimu na kuthamini sheria asilia, maadili na utu wema. Kuna baadhi ya wanahakati ndani ya Jamii wanataka kujichukulia sheria mikononi mwao wa kuwa ni vipimo na vigezo vya maadili na misimamo ya kijamii hata pale wanapokuwa wamepotoka na kukengeuka, jambo ambalo kamwe haliwezi kukubalika!

Kanisa haliwezi kukubali kushinikizwa kufungisha ndoa za watu wa jinsia moja kwa mfano kwani hiki ni kinyume kabisa cha Maandiko Matakatifu, maadili na utu wema. Ni jambo linalokwenda kinyume na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu anayeshirikishwa katika mchakato wa kuzaa na kulea watoto. Kanisa haliwezi kupindisha Mafundisho yake ili kupata msaada wa fedha zenye masharti kama inavyojionesha kwa baadhi ya nchi na wahisani wanaotaka kuzilazimisha nchi za Kiafrika kupitisha sheria zinazokumbatia utamaduni wa kifo kwa kisingizio cha uhuru na demokrasia na kusahau kwamba, hata uhuru una mipaka na ukomo wake!

Askofu mkuu Kaigama ambaye pia ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria amewataka Wananchi wa Nigeria na Afrika katika ujumla wao, kuwa makini na athari za utandawazi zinazoweza kuwachanganya na kuwavuruga kiasi cha kushindwa kutambua kama kweli ni Waafrika au wamekwishagenishwa kwa tamaduni za kigeni ambazo baadhi yake zimepotoka na kukengeuka! Waamini wawe waaminifu na wadumifu katika Mapokeo ya dini zao, mila na desturi njema za Kiafrika. Wabnanchi hawapaswi kuiga kila jambo analotenda mtu kutoka Ulaya.

Wafanyakazi katika sekta ya afya wanapaswa kulinda na kutetea: maisha, utu na heshima ya binadamu na kamwe wasikumbatie utamaduni wa kifo! Waongozwe na kanuni bora za maadili na sheria za kazi pamoja na kujitabisha kujifunza kanuni msingi za Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Madaktari na wauguzi waendelee kutoa huduma hali wakibaki kuwa ni Wakatoliki waaminifu, waadilifu na wachapa kazi, mfano wa kuigwa na wafanyakazi wengine katika huduma za kijamii, kwa njia hii watakuwa wanayatakatifuza malimwengu kwa njia ya maisha na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.







All the contents on this site are copyrighted ©.