2014-02-15 15:19:12

Kuna haja ya kujenga utamaduni wa amani na majadiliano kwa ajili ya mafao ya wengi!


Rais Nikos Anastasiades wa Cyprus anasema, kuna haja kwa nchi zinazozunguka Bahari ya Mediterania kujenga na kuimarisha utamaduni unaojikita katika misingi ya haki na amani pamoja na majadiliano yanayolenga mafao ya wengi. Kuna maelfu ya watu wanaotafuta njia za kufika Ulaya kutokana na makali ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa, majanga asilia, vita na kinzani za kijamii na kisiasa. Watu hawa wanapaswa kusaidiwa kwa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao na zaidi ya hayo kukuza utamaduni wa ukarimu kwa wageni.

Kwa bahati mbaya haya ni mambo yanayoonekana kana kwamba, hayana thamani tena katika misingi ya maisha ya kijamii na badala yake nchi nyingi zinaendekeza sera za kibaguzi na kinzani za kidini. Waamini wa dini ya Kikristo na Kiislam kwa miaka mingi waliishi kwa amani na utulivu nchini Cyprus. Chochoko za Mwaka 1974 zilizojikita katika udini na ukabila zimepelekea mnafarakano kati ya Wakristo na Waislam nchini humo.

Cyprus ni daraja la watu wanaotoka Asia na Afrika kuelekea Ulaya. Hii ni nchi yenye watu wenye imani na tamaduni tofauti, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu sanjari na uhuru wa kidini.

Rais Nikos Anastasiades wa Cyprus anasema, Jumuiya ya Kimataifa haina budi kushikamana kwa dhati ili kuhakikisha kwamba, mgogoro wa kivita nchini Syria unaoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao unapata ufumbuzi wa kudumu kwa kuzingatia na kuheshimu mafao ya wengi. Biashara ya silaha nchini Syria inayofanywa na baadhi ya nchi pamoja na makampuni makubwa ya silaha haina budi kusitishwa ili kuokoa maisha ya watu wasiokuwa na hatia yanayoendelea kupukutika siku hadi siku.

Cyprus inaunga mkono juhudi za Vatican katika kulinda na kutetea haki za wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Kimataifa ikishikamana kwa dhati, biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo vinaweza kukomeshwa, kwa kuheshimu sheria na haki msingi za binadamu. Jumuiya ya Kimataifa ibainishe mambo yanayopelekea kuwepo na kushawimiri kwa biashara haramu ya binadamu na hivyo kuyatafutia ufumbuzi wa kudumu. Serika na mikakati ya Jumuiya ya Ulaya hazina budi kusoma alama za nyakati kwa ajili ya utekelezaji wa mafao ya wengi, utulivu na amani duniani.

Jumuiya ya kimataifa inaendelea kuonja athari za myumbo wa uchumi kimataifa kwa ukosefu wa fursa za ajira, hali ngumu ya maisha na watu kuanza kukata tamaa kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha wakati hali ya maisha inazidi kuporomoka siku hadi siku.

Cyprus imeguswa na kutikiswa na athari za myumbo wa uchumi kimataifa, lakini imefanikiwa kujinasua huko kutokana na msaada kutoka katika Jumuiya ya Kimataifa, vinginevyo, Serikali ya Cyprus ingetangazwa kwamba, imefilisika na wala haikopesheki tena! Serikali inaendelea kujifunga mkanda ili kukabiliana na athari za myumbo wa uchumi kimataifa na sasa hali inaanza kubadilika.







All the contents on this site are copyrighted ©.