2014-02-15 15:07:52

Kumbu kumbu ya Miaka 30 ya mabadiliko katika Muafaka wa Laterano: lengo ni uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu!


Serikali ya Italia na Vatican wanasherehekea kwa pamoja miaka 30 tangu Muafaka wa Laterano ulipofanyiwa marekebisho makubwa kunako tarehe 18 Februari 1984 kwa kutambua umuhimu wa Kanisa na Serikali kushirikiana, lakini kila upande ukitekeleza majukumu yake bila kuingiliana, kwa ajili ya mafao ya wengi na maendeleo ya wananchi wa Italia.

Huu ni ushirikiano unaojikita katika misingi ya ukweli na uwazi; urafiki na ukomavu; amani na utulivu hasa ukizingatia kwamba, Kanisa Katoliki nchini Italia limelipa gharama kubwa kutokana na mauaji ya watoto wake!

Yote haya ni matunda ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Sheria Mpya za Kanisa zilizopitishwa na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili kunako mwaka 1984 na hivyo Vatican na Serikali ya Italia wakalazimika kupitia tena Muafaka wa Laterano uliokuwa umetiwa sahihi kunako mwaka 1929, lakini bado kulikuwa na hali ya kudhaniana vibaya pamoja na uhasama wa kisiasa.

Kwa muhtasari huu ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Kardinali mteule Pietro Parolin, Katibu mkuu wa vatican katika Warsha iliyokuwa imeandaliwa kwa ajili ya kufanya kumbu kumbu ya miaka thelathini tangu Serikali ya Italia na Vatican walipofanya marekebisho makubwa kwenye Muafaka wa Laterano kwa kukazia: uhuru wa kidini, utu na heshima ya binadamu pamoja na mafao ya wengi. Haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama yanavyofafanuliwa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Kardinali mteule Parolin anasema, Kanisa linajitambua kuwa ni Familia ya Mungu inayopenda kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kumwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili hasa katika sekta ya Uinjilishaji Mpya, Elimu, Afya na Maendeleo endelevu; utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.







All the contents on this site are copyrighted ©.