Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ni daraja kati ya Serikali na Vatican
Kanisa na Serikali vinaweza kushirikiana kwa karibu katika masuala ya uchumi bila
ya kinzani wala kutazamana kwa "macho ya makengeza". Ili kufanikisha mchakato huu,
kuna haja kwa Kanisa kuwa na sera na mikakati sahihi ya kiuchumi inayopania pamoja
na mambo mengine kuhakikisha kwamba, inaboresha maisha ya watu: kiroho na kimwili.
Mshikamano wa upendo unaoongozwa na kanuni auni ni muhimu sana kwa ajili ya ustawi
na maendeleo ya watu sehemu mbali mbali za dunia.
Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican pamoja na Sheria za Kanisa za Mwaka 1984 zimeweka vipaumbele vya ushirikiano
wenye tija na mashiko kati ya Serikali na Kanisa Katoliki kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya wengi. Utekelezaji wa sheria na Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa
Vatican unafanywa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika nchi husika, kwa kuongozwa
na kanuni auni; mambo msingi katika Mafundisho Jamii ya Kanisa.
Askofu Nunzio
Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia akichangia mada kwenye
Kongamano la Siku moja kuhusu Maadhimisho ya Miaka thelathini tangu Serikali ya Italia
na Vatican walipofanya marekebisha msingi katika Muafaka wa Laterano anasema kwamba,
utekelezaji wake kimsingi unafanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Kumekuwepo
na ushirikiano wa karibu kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki kuhusiana na
masuala ya fedha na uchumi.
Sehemu ya kodi inayotolewa na wananchi wa Italia
inatumika kwa ajili ya kugharimia maisha na utume wa Kanisa ndani na nje ya Italia.
Serikali pia imeanzisha mfumo kwa ajili ya kutoa ruzuku kwa Mapadre wanaowahudumia
wananchi wa Italia: kiroho na kimwili.
Baraza la Maaskofu Katoliki Italia
linawajibika kutoa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za walipa kodi nchini Italia
kwa serikali, jambo linaloonesha uwajibikaji wa pamoja kwa ajili ya mafao ya wengi.
Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia
anasema, kimsingi Baraza la Maaskofu Katoliki Italia ndilo daraja kuu kati ya Serikali
ya Italia na Vatican katika utekelezaji wa Muafaka wa Laterano unaoadhimisha Miaka
thelathini tangu ulipofanyiwa marekebisho.