2014-02-14 08:18:20

Mwaka 2014 ni Mwaka wa Mawasiliano Jamii nchini India


Baraza la Maaskofu Katoliki India limeamua kwamba Mwaka 2014 ni Mwaka wa Mawasiliano Jamii nchini Hindia kama kielelezo cha kumbu kumbu ya Miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipochapisha Hati kuhusu Mawasiliano ya Jamii, Inter Mirifica. RealAudioMP3

Lengo la Kanisa Katoliki nchini India ni kutaka kuhamasisha mikakati na shughuli za kichungaji katika njia za mawasiliano ya jamii, ili Jamii iweze kuwasiliana kwa kuzingatia kanuni maadili; ukweli na uwazi; weledi na mafao ya wengi; mambo ambayo wakati mwingine yanapuuzwa na vyombo vya upashanaji habari.

Mwaka wa Mwasiliano ya Kijamii nchini India utapambwa na Kongamano la Kimataifa kuhusu njia za mawasiliano ya Kijamii; Siku ya Mawasiliano Kitaifa, Semina mbali mbali zitakazofanyika katika ngazi mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa nchini India.

Askofu Chako Thottumarikali, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki India anasema, Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walilihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linashiriki kikamilifu katika matumizi makini ya vyombo vya mawasiliano ya Jamii kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Hati ya Inter Mirifa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu wa njia za mawasiliano ya kijamii.

Nyaraka nyingine zilizotolewa na Viongozi wakuu wa Kanisa zimeendelea kufanya rejea katika waraka huu, hasa kwa kuzingatia maendeleo makubwa yaliyokwisha kupatikana katika ulimwengu wa sayansi na njia za mawasiliano ya kijamii. Baraza la Maaskofu Katoliki India linapenda kuwahamasisha waamini na wananchi katika ujumla wao, kushiriki kikamilifu katika matumizi ya njia za mawasiliano ya kijamii kwa ajili ya kutangnaza Injili ya Furaha sehemu mbali mbali za dunia.

Utangazaji wa Injili kwa njia mbali mbali za mawasiliano ya kijamii ni sehemu ya vinasaba vya Kanisa Katoliki; waamini na watu wenye mapenzi mema, wapokee changamoto hii na kuifanyia kazi ili Injili ya Kristo iweze kuwafikia watu wengi zaidi.








All the contents on this site are copyrighted ©.