2014-02-14 14:44:31

Maswali yaliyoulizwa na wanandoa watarajiwa kwa Papa Francisko


Katika Maadhimisho ya Siku ya Wapendao Duniani kwa Mwaka 2014, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wanandoa watarajiwa 20, 000 kutoka katika nchi 28, waliokusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, ambao ulipambwa na kupambika kwa sura za vijana wanaopendana, vijana ambao wanataka kufunga pingu za maisha, ili kufurahia maisha hadi pale kifo kitakapowatenganisha.

Wanandoa wamemwambia Baba Mtakatifu Francisko kuhusu: furaha ya maisha ya ndoa, wasi wasi na mashaka yaliyomo mioyoni mwao. Uaminifu hadi kifo kitakapowatengenanisha ni kati ya changamoto kubwa iliyoko mbele yao kutokana na ukweli kwamba, hata katika maisha ya ndoa na familia bado kuna usaliti mkubwa ambao unapelekea ndoa nyingi kuvunjika au kukosa mwelekeo.

Vijana wamemwambia Baba Mtakatifu kwamba, kati yao walikutana kwa mara ya kwanza wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Madrid, Hispania, kila mtu akiwa amebeba ndani mwa begi lake: sala, matumaini, udadisi na maswali yasiyokuwa na majibu. Walionana, wakapendana na sasa wanataka kufunga ndoa Kanisani, ili kujenga familia ambayo kimsingi ni Kanisa dogo la nyumbani. Vijana wanataka kusikia kutoka kwa Baba Mtakatifu: mtindo wa maisha ya ndoa na familia ya Kikristo; tasaufi ya maisha ya ndoa katika ujumla wake.

Wanandoa watarajiwa wamezungumzia kuhusu ushiriki wao mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Baada ya kufahamiana, sasa wanasubiri kwa hamu kubwa ile siku watakaposimama mbele ya Altare ili kufunga ndoa, kwa kuwa na kiasi pasi na kutaka makuu; kwa kuonesha mshikamano wa upendo na maisha ya kujisadaka kwa ajili ya wengine, kwa kutambua pia athari za myumbo wa uchumi kimataifa ambao umekuwa ni kikwazo kikubwa kwa vijana wengi kufunga ndoa Kanisani. Ni vijana wenye matumaini makubwa, lakini kuna wajanja wachache wanaotaka kuwapokonya matumaini yanayojikita mioyoni mwao!







All the contents on this site are copyrighted ©.