Epukeni kishawishi cha kugeuka na kuwa ni Mbwa mwitu badala ya Kondoo!
Baba Mtakatifu Francisko katika Ibada ya Misa Takatifu, kumbu kumbu ya Watakatifu
Cyril na Metodi, iliyofanyika kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini
Vatican, Ijumaa tarehe 14 Februari 2014 amewakumbusha waamini kwamba, wanatumwa kama
Kondoo kati ya Mbwa mwitu na kamwe wasigeuke na kuanza wao wenyewe kuwa ni Mbwa mwitu,
kinyume cha agizo la Kristo. Injili ya Kristo inatangazwa kwa furaha na wala litania
ya malalamiko haina nafasi.
Wakristo wanakumbushwa kwamba, wameitwa na kutumwa
na Kristo kutangaza Injili ya Furaha kila pembe ya dunia wakitambua kwamba, njiani
watakumbana na "majanga" ya maisha, lakini hawana sababu ya kuogopa, lakini bado waendelee
kutunza utambulisho wao wa Kikristo. Kamwe waitumbukie katika kishawishi cha kugeuka
na kuwa Mbwa mwitu, kwani Kristo anaweza kuwatema na kuwaacha soremba!
Furaha
ni sehemu ya utambulisho wa maisha ya Mkristo, kwani ni kielelezo kwamba wamekutana
na kuonana na Yesu, ambaye ni sababu ya furaha ya maisha yao. Katika shida na mahangaiko
yao, Yesu yuko pamoja nao na yuko tayari kuwasaidia, kumbe Injili ya Kristo haina
budi kusonga mbele kwa kushuhudiwa kwa njia ya furaha; huzuni na masikitiko yanachafua
utambulisho huu wa Wakristo.