Licha ya madhulumu na nyanyaso za kidini wakati wa Ukomunisti, lakini Kanisa nchini
Bulgaria kuwa kielelezo cha ushuhuda wa imani na mapendo
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 13 Februari 2014 amekutana na kuzungumza
na Maaskofu Katoliki Bulgaria ambao wako mjini Vatican katika hija ya kitume inayofanyika
walau kila baada ya miaka mitano. Amewapongeza kwa ushuhuda wa imani na mapendo unaooneshwa
na Wakristo nchini Bulgaria.
Papa amewapongeza pia kwa Maadhimisho ya Jubilee
ya Miaka 150 ya uhusiano kati ya Bulgaria na Vatican, yaliyofanyika kunako mwaka 2010;
Kumbu kumbu ya Miaka 60 tangu Mwenyeheri Evgenij Bossilkov alipouwawa kikatili pamoja
na Maadhimisho mbali mbali sanjari na Mwaka wa Imani. Maadhimisho yote haya yanaonesha
ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya kimaadili na Kikristo, licha ya madhara makubwa
yaliyosababishwa na nyanyaso za kidini kutokana na utawala wa Kikomunisti.
Changamoto
iliyoko mbele yao kwa sasa ni kujikita katika mchakato wa maisha ya kimissionari unaofanyiwa
kazi na Mama Kanisa kwa wakati huu, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya
Ubatizo, Wakristo wote wanatumwa kutangaza Injili kwa furaha na kwa moyo mkuu pamoja
na kuthamini Ibada mbali mbali zinazofanywa na waamini, bila kusahau kumwilisha Mafundisho
Jamii ya Kanisa katika maisha na vipaumbele vya waamini; kwa kupambana na baa la umaskini,
daima wakisimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, haki na amani. Kanisa litaendelea
kuchangia katika ustawi na mafao ya wengi nchini Bulgaria, kwa kuheshimu uhuru wa
kidini.
Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu Katoliki Bulgaria kujikita
katika majiundo endelevu kwa waamini walei kwa njia ya Katekesi, utume miongoni mwa
vijana pamoja na kulea na kukuza miito mitakatifu ndani ya Kanisa, kama kielelezo
cha ukomavu wa imani na changamoto ya kimissionari. Maaskofu waendeleze mchakato wa
majadiliano ya Kiekumene na Kanisa la Kiorthodox; kwa kusali na kutafakari kwa pamoja
Neno la Mungu, ili siku moja waweze kuadhimisha kwa pamoja Fumbo la Ekaristi Takatifu,
kielelezo cha umoja kamili kati ya Wakristo.
Baba Mtakatifu Francisko amewapongeza
waamini kutoka Bulgaria wanaotarajia kushiriki kwa wingi katika Ibada ya kuwatangaza
watakatifu Mwenyeheri Yohane wa XXIII na Yohane Paulo II hapo tarehe 27 Aprili 2014.
Hawa ni watu walioacha chapa ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa nchini Bulgaria;
wakaacha taa ya imani inayoendelea kuwaka hadi leo hii.