2014-02-12 08:18:50

Mradi wa miaka 5 kwa ajili ya huduma kwa waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi wazinduliwa nchini Tanzania


Mfuko wa Msamaria mwema, unaosimamiwa na Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya kwa kushirikiana na Idara ya afya ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Kampuni ya Gilead Sciences kutoka Marekani, wamekubaliana kimsingi kusaidia juhudi za kupambana na ugonjwa wa Ukimwi mkoani Shinyanga, kwa kusaidia juhudi za kupima virusi vya Ukimwi kwa wananchi 120, 000 pamoja na kuwapatia dawa za kurefusha maisha wale watakaokuwa wameathirika.

Makubaliano hayo yamefikiwa Jijini Dar es Salaam, tarehe 11 Februari 2014 katika Maadhimisho ya Siku ya 22 ya Wagonjwa Duniani. Huu ni mradi wa miaka mitano kwa ajili ya kupima virusi vya Ukimwi na kutoa dawa za kurefusha maisha. Ni mradi unaozingatia taaluma, maadili, usafi pamoja na mafunzo kwa walengwa watakaofaidika na mradi huu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa watoto yatima.

Mradi huu utaendelea kuongeza nguvu katika kuwahudumia wagonjwa wa Ukimwi, juhudi zinazofanywa na Jimbo Katoliki la Shinyanga katika Vituo vya Afya vya: Ngokolo, Bugisi, Buhangija na Mija. Mradi utatoa ufadhili kwa ajili ya mafunzo ya hali ya juu kwa wahudumu wa sekta ya afya, ili kuweza kutekeleza wajibu wao barabara pamoja na kuendelea kujikita katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi na maambukizi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto.

Wananchi watakaogundulika kuwa na maambukizi ya Ukimwi watapewa dawa za kurefusha maisha anasema Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya. Mradi unapania pamoja na mambo mengine, kudhibiti maambukizi ya virusi kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto, kama sehemu ya huduma makini inayotolewa na Kanisa katika kumhudumia mtu mzima: kiroho na kimwili, kama sehemu ya mwendelezo wa agizo la Kristo katika kuwahudumia wagonjwa.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, amemkumbuka kwa namna ya pekee, Marehemu Askofu Aloysius Balina wa Jimbo Katoliki Shinyanga, aliyefariki dunia mwezi Novemba 2012. Aliamini kuhusu mafanikio ya mradi huu katika kuwahudumia watanzania waliokuwa wameathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi. Ni mradi wa pekee, unaojumuisha Mfuko wa Msamaria Mwema, Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya pamoja na Kampuni ya Gilead.

Lengo li kuhakikisha kwamba, Kanisa Katoliki linashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ukimwi ambao umekuwa ni chanzo cha vifo na upotevu wa nguvu kazi nchini Tanzania.

Maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, yalianzishwa kunako mwaka 1992 na Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, ambaye hapo tarehe 27 Aprili 2014 anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu. Siku ya Wagonjwa Duniani inalenga pamoja na mambo mengine kuhakikisha kwamba, wagonjwa wanapata huduma bora pamoja na kuishirikisha Familia ya Mungu katika huduma kwa wagonjwa, kwani wagonjwa bado wanayo nafasi ya pekee katika maisha na utume wa Kanisa.

Kanisa linawahamasisha watu wa kujitolea, ili waweze kuwashirikisha jirani zao upendo, kwa kuwaonjesha upendo. Kanisa linapania pia kutoa majiundo makini ya kitaaluma na kimaadili kwa wahudumu wa sekta ya afya.







All the contents on this site are copyrighted ©.