2014-02-12 14:55:19

Jengeni uwiano bora kati ya adhimisho la Ekaristi Takatifu, Liturujia na maisha ya Kikristo!


Fumbo la Ekaristi Takatifu linamwingiza mwamini katika mchakato wa kukutana na Yesu katika Fumbo la Pasaka, chemchemi ya upendo na neema inayobubujika kutoka katika: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya waamini ni kuangalia ni kwa jinsi gani wanavyomwilisha Adhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Ibada ya Misa Takatifu, ni Sherehe endelevu inayomwezesha mwamini kushibishwa kwa Neno la Mungu na Mkate wa uzima ulioshuka kutoka mbinguni; mambo yanayomwezesha mwamini kufanana na Kristo, changamoto na mwaliko wa kubadilika.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 12 Februari 2014, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wakati wa Katekesi yake ambayo kwa wakati huu inalenga juu ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kielelezo cha upendo wa Kristo aliyejisadaka pale Msalabani, ili kumwonjesha mwanadamu upendo wa Kimungu, mwaliko kwa waamini kuwamegea wengine pia upendo, kwa kuguswa na shida pamoja na mahangaiko ya jirani zao.

Ekaristi Takatifu ijenge na kuimarisha mshikamano kati ya waamini; tayari kufurahi na wale wanaofurahia; kuhuzunika na wale wanaohuzunika katika maisha yao; tayari kujisadaka kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili kutambua sura ya Kristo inayojionesha miongoni mwa watu hawa!

Baba Mtakatifu anasema, Ekaristi Takatifu inamwezesha mwamini kupata neema ya msamaha, tayari kusamehe. Waamini wanaposhiriki katika Ibada ya Misa Takatifu wanatambua kwamba, wanaweza kupokelewa na hatimaye, kuonja huruma ya Mungu inayojionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Yesu Kristo.

Waamini wanakumbushwa kwamba, Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ilianzishwa na Yesu mwenyewe, usiku ule ulioatangulia kuteswa kwake baada ya kusalitiwa, mwaliko kwa waamini kutubu na kuongoka. Ekaristi Takatifu inawakirimia waamini neema ya msamaha wa dhambi; muhtasari wa sadaka ya Kristo Msalabani, tayari kusamehe na kuwapatanisha watu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga uhusiano wa dhati kati ya Adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu na maisha ya Jumuiya za Kikristo, kwani Ekaristi Takatifu ni tendo na zawadi ya Kristo kwa waja wake, wanaolishwa kwa Neno na maisha yake na kwamba, utume na maisha ya Kanisa yanapata chimbuko lake kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Maadhimisho haya yawawezeshe waamini kukutana na Yesu Kristo anayeshibisha roho na maisha yao. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu Yesu anapenda kuingia katika maisha ya waamini ili kuwapatia neema, mwaliko kwa Jumuiya za Kikristo kuwa na uwiano bora kati ya Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Liturujia na Maisha. Kwa mwamini anayeshiriki Fumbo la Ekaristi takatifu atambue kwamba, anakula Mwili na kunywa Damu azizi ya Yesu ambaye atamfufua siku ya mwisho.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanaliishi Fumbo la Ekaristi Takatifu kwa moyo wa imani na sala, wakiwa na matumaini kwamba, Yesu atatekeleza yale ambayo amewaahidia wafuasi wake. Anawaalika vijana kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu kila Jumapili, ili Yesu aweze kuwasaidia kufanya mabadiliko katika maisha yao.

Waamini wawe ni mashahidi wa upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Waamini wasiwe na woga wa kujisadaka, kuwashirikisha na kuwapenda jirani zao. Baba Mtakatifu Francisko ametambua uwepo wa Maaskofu kutoka Jamhuri ya Watu wa Ceco wanaofanya hija ya kitume mjini Vatican.

Tarehe 14 Februari, Kanisa litaadhimisha Siku kuu ya Watakatifu Cyril na Metodi, Wasimamizi wa Bara la Ulaya. Usuhuhuda wa maisha na utume wao wa Kimissionari uwachangamotishe vijana kuwa ni mitume na wamissionari; wagonjwa watolee shida na mahangaiko yao kwa ajili wongofu wa wadhambi; wanandoa wapya wahakikishe kwamba, Injili inakuwa ni mwongozo na kanuni ya maisha yao ya kifamilia.







All the contents on this site are copyrighted ©.