2014-02-12 08:59:52

Cor Unum na mshikamano wa upendo kwa waathirika wa maafa asilia nchini Haiti, Guatemala na Ufilippini


Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum katika mikakati yake ya huduma ya upendo na mshikamano, linawalenga hasa waathirika wa maafa asilia nchini Haiti, Ufilippini na Guatemala ambako kutafanyika uzinduzi wa makazi ya watu yaliyojengwa na Cor Unum.

Hayo yamebainishwa na Kardinali Robert Sarah, Rais wa Cor Unum katika utekelezaji wa huduma kwa waathirika wa maafa asilia si tu wakati wa dharura bali kwa kuwa na mikakati ya muda mrefu.

Mwezi Machi 2014, Kardinali Sarah atakabidhi nyumba 19 kwa wananchi wa Guatemala walioathirika kutoka na mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo mwezi Agosti 2013. Wananchi hawa watapata makazi ya kudumu pamoja na kuendelea kuonesha kwamba, Kanisa linatoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya kifamilia, kwa kuwajengea watu uwezo wa kuishi katika hadhi pamoja na kuheshimu haki msingi za maisha ya ndoa na familia.

Nchini Haiti, Cor Unum imejenga shule kwa kushirikiana na Ubalozi wa Vatican nchini Haiti, kielelezo cha mshikamano wa upendo na wananchi wa Haiti ambao hivi karibuni walikumbwa na tetemeko la ardhi na hivyo kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Kanisa limekuwepo na litaendelea kuwaunga mkono wananchi wa Haiti katika shida na mahangaiko yao.

Zaidi ya wananchi elfu tano walipoteza maisha kutokana na tufani iliyokumba Ufilippini tarehe 8 Novemba 2013. Kuna idadi kubwa ya watu ambao wamepoteza makazi yao na wanahitaji msaada wa dharura, Cor Unum inapenda kuwahakikishia wananchi wa Ufilippini kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameyaona na kusikiliza kilio chao na yuko tayari kuwashika mkono ili kuwasaidia kupata matumaini mapya katika maisha, kwa kuendelea kushirikiana na Kanisa mahalia.

Cor Unum ina bainisha kwamba, Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia yamekuwa ni msaada mkubwa katika kuwahudumia watu wanaokumbwa na maafa asilia na kwamba, Cor Unum inapotembelea katika maeneo haya, inapania pamoja na mambo mengine kuainisha miradi ya muda mrefu inayoweza kufanyiwa kazi kwa ajili ya mafao ya wananchi husika.

Kardinali Robert Sarah hivi karibuni alifanya ziara ya kikazi nchini Ufilippini na kupata nafasi ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katokiki Ufilippini lililokuwa linaadhimisha Mkutano wake wa kawaida. Akiwa nchini humo, Kardinali Sarah amewatafakarisha Maaskofu kuhusu Taalimungu ya Upendo, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, changamoto endelevu kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa.

Waamini wanapaswa kutambua kwamba, huduma ya upendo kama alivyosema Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita ni sehemu ya vinasaba vya Mama Kanisa. Huduma ya upendo inapata chimbuko lake kutoka katika asili na utume wa Kanisa. Waamini wanachangamotishwa kushiriki kikamilifu katika kuwaonjesha jirani zao upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hata katika shida na mahangaiko ya watu, hapo imani inaweza kukua na kukomaa.

Cor Unum nchini Ufilippini imekwisha bainisha miradi mikuu mitatu: Kituo cha Watoto Yatima kwa ajili ya kuwapokea na kuwahudumia watoto yatima: kiroho na kimwili. Hawa ni wale watoto ambao wazazi wao wamefariki dunia kutokana na tufani iliyoikumba nchi ya Ufilippini.

Mradi wa pili ni ujenzi wa Kituo cha Wazee ambao kwa sasa wanahitaji msaada wa hali na mali baada ya kuondokewa na wale waliokuwa wanawatunza na kuwapatia msaada. Mradi wa tatu ni ujenzi wa kituo cha afya kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Ufilippini. Hiki ni kielelezo makini cha imani tendaji!







All the contents on this site are copyrighted ©.