Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 2013, Baba Mtakatifu Benedikto wa kumi na sita, alipotangaza
rasmi kwamba, kwa hiyari yake mwenyewe na utashi kamili ameamua kung'atuka kutoka
madarakani, ili kutoa nafasi kwa Makardinali kuweza kumchagua Khalifa mwingine wa
Mtakatifu Petro.
Maneno haya
yakaushangaza ulimwengu. Kwa Kanisa hili likawa ni tukio la kinabii, ili kutoa nafasi
kwa Mama Kanisa kuendelea kufanya mageuzi ya kina katika maisha na utume wake, Mwenyezi
Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza; waamini wakijikita kutangaza Habari Njema ya
Wokovu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Akachaguliwa
Baba Mtakatifu Francisko ambaye ameamua kuendeleza mageuzi yaliyokuwa yameanzishwa
na Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita katika maisha na utume wa Kanisa kwa kukazia
uaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, bila kumezwa na malimwengu, mambo ambayo yamelisababishia
Kanisa kujikuta linaandamwa na kashfa mbali mbali. Maaskofu mahalia wamepewa dhamana
ya kuhakikisha kwamba, wanatekeleza utume wao wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza
watu wa Mungu kwa ujasiri na moyo mkuu.
Kuna waamini ambao bado wana madonda
makubwa katika mioyo yao, jambo la msingi kwa Kanisa ni kujikita katika mchakato wa
uponyaji na upatanisho, ili Kanisa liweze kusonga mbele kwa ari kubwa zaidi katika
azma yake ya kuwatangazia watu Injili ya Furaha.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, aliona kashfa ya matumizi haramu ya fedha iliyokuwa inalinyemelea
Kanisa kwa kutumia migongo ya wajanja wachache ndani ya Kanisa. Vatican ikatunga na
kuridhia sheria inayopiga vita utakatishaji wa fedha haramu inayoweza kutumika kugharimia
vitendo vya kigaidi. Papa Francisko anaendelea kukazia umuhimu na dhamana ya wanawake
katika maisha na utume wa Kanisa.
Kanisa linamshukuru na kumpongeza Papa mstaafu
Benedikto wa kumi na sita, kwa ujasiri na uamuzi wake wa busara wa kung'atuka kutoka
madarakani, ili aweze kupata nafasi kubwa zaidi ya kusali na kutafakari.