2014-02-11 09:28:50

Papa mstaafu Benedikto XVI kwa sasa ana utume wa sala na tafakari; uamuzi wake ni ushuhuda wa kinabii!


Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican, anabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita kwa sasa anautumia muda wake mwingi kwa ajili ya kusali na kutafakari na kwamba, uamuzi wake wa kung'atuka kutoka madarakani ni wazo ambalo alilitafakari, akasali na kulipembua kwa kina na mapana yake, hatimaye, akafikia uamuzi wa kinabii wa kung'atuka kutoka madarakani.

Ni uamuzi ambao umeacha chapa ya kudumu katika historia, maisha na utume wa Kanisa. Papa mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alitafakari na kujiandaa kwa hali ya utulivu kuweza kuanza upya hija ya maisha yake ya kiroho, kwa kuendelea kulisindikiza Kanisa katika maisha na utume wake kwa njia ya Sala. Makardinali wakamchagua Papa Francisko kuliongoza Kanisa na hapo mchaka mchaka ukaanza kwa kasi na ari ya ajabu, kiasi cha kuvunjilia mbali wasi wasi kuhusu uwepo wa Mapapa wawili ndani ya Kanisa.

Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alitambua kwamba, uongozi ni dhamana na huduma kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Padre Lombardi anasema, Papa Benedikto wa kumi na sita, mara kwa mara alikuwa anampatia Rozari au medali, akimkumbusha kwamba, hata Mapadre wanapaswa kusali ili waweze kutekeleza wajibu na dhamana yao kwa Kristo na Kanisa lake. Sala na tafakari ni utume unaoendelezwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita.

Baba Mtakatifu mstaafu anaendelea na maisha yake ya uzee, anakutana na watu walio karibu naye na kujibu barua mbali mbali anazoandikiwa na watu; bado anaendelea kutoa ushauri pale unapohitajika. Mara kadhaa amekutana na kuwasiliana na Papa Francisko, kielelezo cha mshikamano wa upendo, kwani hii ni huduma ya Kanisa la Kristo na wala si ujiko wa mtu binafsi! Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ataendelea kukumbukwa kuwa ni kati ya Wazee wa Kanisa; watu waliosheheni: hekima, busara na imani.

Padre Lombardi anasema, licha ya sifa zote hizi, bado anaweza kuitwa Mtakatifu wa Mungu, mwaliko wa kuwa na utulivu wa ndani na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu, tayari kusonga mbele katika hija ya imani na matumaini.







All the contents on this site are copyrighted ©.