Serikali ya Italia na Vatican kwa pamoja zinafanya kumbu kumbu ya Miaka 85 tangu nchini
hizi mbili zilipowekeana sahihi katika Muafaka wa Laterano na kufanyiwa marekebisho
ya msingi mintarafu Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Sheria Mpya za Kanisa kunako
tarehe 18 Februari 1984, miaka thelathini iliyopita.
Muafaka huu umezingatia
maisha na utume wa Kanisa mintarafu mabadiliko ya kisiasa, kijamii, kiuchumi na kitamaduni
nchini Italia. Muafaka huu umekuwa ni Waraka rejea wa mahusiano kati ya Vatican na
nnchi mbali mbali duniani.
Muafaka unakubaliana kimsingi kwamba, Kanisa halichangamani
katu na Jumuiya ya kisiasa, wala haifungamani na mtindo wowote wa mfumo wa kisiasa
kwa sababu ya majukumu na uhalali wake. Serikali na Kanisa zina uhuru na mamlaka kila
mmoja katika uwanja wake, zote mbili zipo kwa ajili ya kumtumikia mwanadamu. Serikali
ya Italia inalitambua Kanisa Katoliki katika utekelezaji wa maisha na utume wake kwa
uhuru kamili bila ya kuingiliwa katika shughuli za kichungaji, elimu, matendo ya huruma,
ibada na katika dhamana yake ya kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Muafaka huu umeliwezesha
Kanisa Katoliki nchini Italia kuwa karibu na wananchi katika shida, mahangaiko, furaha
na matumaini yao, kwa kuendelea kuhimiza misingi ya maadili na utu wema, mambo msingi
katika kukuza na kudumisha demokrasia ya kweli. Kanisa limeendelea kuchagia katika
ustawi na maendeleo ya wengi nchini Italia katika medani mbali mbali za maisha kwa
kutumia utajiri mkubwa unaofumbatwa katika Mashirika mbali mbali ya kitawa na kazi
za kitume. Kimsingi muafaka huu ni kwa ajili ya maendeleo ya mtu mzima na mafao ya
wengi.