2014-02-10 10:29:48

Mshikamano wa dhati na wasichana wanaoishi kwenye mazingira hatarishi


Kikundi cha wake wa Viongozi (Millenium Women Group) kimetoa msaada wa Chakula, Mavazi na Vifaa vya usafi vyenye thamani ya sh. Milioni 6.8/- kwa “New Hope for Girls Organization’’ kinacholea wasichana wanaoishi katika mazingira magumu.

Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda alieleza kuwa, wake wa viongozi waliguswa baada ya kukutana na Bibi. Consoler Eliya mwaka jana katika mkutano wa wanawake wajiwezeshe kiuchumi ambaye ni miongoni mwa wasichana walioishi katika mazingira magumu na kuahidi kumsaidia.


Misaada hiyo ilitolewa kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay, jijini Dar es Salaam “Akina mama wameona jitihada za Bibi. Consoler katika kusaidia wasichana hawa wanaoishi katika mazingira magumu, ambayo watu wengi wamekuwa wakiyapitia na kushindwa kujitolea kama ilivyokuwa kwa Bibi. Consoler’’,alisema.

Mama Pinda aliongezea kuwa, nia ya Serikali ni kuhakikisha watoto husasani wakike wanaishi kwa amani na kupata haki zao za msingi kwani maisha yao yamekuwa ya huzuni kubwa mno.

Baada ya makabidhiano hayo, Bibi Consoler Eliya, aliwashukuru sana wake wa viongozi kwa msaada waliotoa: “mhitaji si lazima awe yatima, mhitaji anaweza kuwa na wazazi wote na bado akawa anaishi katika mazingira magumu hivyo sisi tunaishi na watoto walitoka katika makundi tofauti ya mazingira magumu’’ alisema. Mbali na kulelewa katika kituo hicho, pia wasichana hao wanabuni na kutengeneza vitu kama batiki, mikufo ambayo inasaidia kuendesha maisha yao, aliongezea Bibi. Consoler.

Mwenyekiti wa kikundi hicho Mama Lukuvi aliongezea kuwa, kutokana na juhudi zinazooneshwa na wasichana hao Kikundi kitawawezesha meza katika mkutano wa wajasiriamali utakaofanyika hivi karibu Jijini Dar es Salaam ili waweze kupeleka bidhaa zao za ubunifu wanazozitengeneza.

Na Rodrick Minja,
Dodoma.








All the contents on this site are copyrighted ©.