2014-02-10 09:56:12

Mikakati makini ya kichungaji ni chachu ya maisha ya kifamilia!


Uinjilishaji mpya na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia ni kati ya tema zinazoendelea kujadiliwa na Tume ya Familia ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufilippini, kwa kuongozwa na kauli mbiu "mikakati makini ya kichungaji ni chachu ya maisha ya kifamilia". Kimsingi haya ni maneno yanayopata chimbuko lake kutoka katika Injili ya Yohane, pale Yesu anaposema, mchungaji mwema anatoa uhai wake kwa ajili ya Kondoo wake.

Huu ni mkutano unaowashirikisha Makleri na Watawa wanaojihusisha kwa karibu zaidi katika shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, ili kuwahamasisha wanafamilia wengi zaidi kujikita katika tafakari ya kina ya Neno la Mungu, linalomwilishwa katika imani tendaji.

Itakumbukwa kwamba, familia za kikristo ni mahali muafaka pa kurithisha imani na tunu msingi za maisha ya kiutu na kijamii, lakini familia pia zinakabiliana na changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi ili ziweze kustawi na kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa Kanisa na Jamii husika. Wajumbe wanajadili mikakati na mbinu zitakazowawezesha wanandoa kushikamana katika maisha na imani; huku wakiendelea kutolea ushuhuda wa maisha yao ya ndoa na familia katika maisha hadhara.

Ulimwengu wa utandawazi umesheheni utamaduni wa kifo, ubinafsi, uchoyo na mambo ya ukanimungu, bila kusahau sera zinazoendelea kuibuliwa na baadhi ya wanasiasa kinyume cha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Kutokana na ukweli huu, Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Ufilippini limeamua kuwajengea uwezo wadau wa shughuli za kichungaji kwa wanandoa na familia, ili waweze kutekeleza vyema wajibu wao msingi kwa kuziimaarisha familia nchini Ufilippini. Wanandoa wanapaswa kutambua kwamba, wanashikamanishwa katika wito wa ndoa unaojikita katika mapendo kamili.

Wawezeshaji katika mkutano huu wanatoka katika Taasisi ya Familia ya Yohane Paulo II iliyoko mjini Roma. Kati ya mada zinazoendelea kuchambuliwa ni uelewa wa ndoa na familia katika maisha ya binadamu; ndoa mintarafu Maandiko Matakatifu sanjari na Taalimungu ya Mwili wa Binadamu; wito wa ndoa na maadili ya Kikristo; Mwelekeo Jamii wa Familia ya wananchi wa Ufilippini; ndoa za Kikristo; ndoa za Serikali; haki msingi za familia na Waraka wa Dhamana ya Familia ulioandikwa na Mwenyeheri Yohane Paulo II kunako Mwaka 1981. Mkutano huu utahitimishwa kwa tamasha la pamoja kati ya wanandoa watarajiwa sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Wapendanao!







All the contents on this site are copyrighted ©.