2014-02-10 11:50:42

Ibada ya Misa Takatifu inaonesha uwepo endelevu wa Kristo kati ya watu wake!


Waamini wanapaswa kutambua uwepo endelevu wa Mungu wakati wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa na kwa namna ya pekee wakati wa Ibada ya Ekaristi Takatifu. Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu katika Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichopo mjini Vatican, siku ya Jumatatu, tarehe 10 Februari 2014, sanjari na Kumbu kumbu ya Mtakatifu Skolastika, Mtawa na Bikira.

Tangu katika Agano la Kale uwepo wa Mwenyezi Mungu ulijionesha kwa namna ya pekee katika Hekalu ambalo liliheshimiwa na kuthaminiwa na Waisraeli. Mwenyezi Mungu aliendelea kuzungumza na watu wake kwa njia ya Manabii, Makuhani na katika Neno lake. Liturujia ni kitendo kinachomwezesha mwanadamu kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwamini kutakatifuzwa, kumbe, kuna haja ya kuheshimu na kuthamini Liturujia zinazoadhimishwa na Mama Kanisa. Kwa namna ya pekee, Kanisa linatambua uwepo wa Kristo katika maumbo ya Mkate na Divai wakati wa Maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Yesu mwenyewe anaendelea kujisadaka kwa Baba yake wa mbinguni kwa ajili ya ukombozi wa walimwengu. Waamini watambue kwamba, wanapaswa kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu na kamwe si wasikilizaji. Pango la Noeli au Njia ya Msalaba ni viwakilishi vya uwepo wa Yesu, lakini Ibada ya Misa Takatifu inamwonesha Kristo mwenyewe kati ya watu wake.

Waamini watambue kwamba, Liturujia ni muda ambao wanaoutolea kwa ajili ya Mungu, mwaliko wa kuwa watulivu na kushiriki kikamilifu katika Ibada, ili kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu Mafumbo ya Mungu katika maisha ya mwanadamu. Ibada ya Misa Takatifu inapaswa kupewa heshima yake katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Ekaristi Takatifu ni kiini na kilele cha maisha na utume wa Kanisa.

Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa yawawezeshe waamini kuingia katika Mafumbo ya Mungu, kwa kutambua utakatifu unaofumbatwa katika Maadhimisho haya. Waamini watofautishe kati ya Ibada ya Rozari Takatifu, Tafakari ya Neno la Mungu au Njia ya Msalaba na Ibada ya Misa Takatifu.







All the contents on this site are copyrighted ©.