Changamoto inayofanyiwa kazi na Sekretarieti ya Vatican katika maisha na utume wa
Kanisa!
Sekretarieti ya Vatican inapaswa kuwa mstari wa mbele katika mchakato wa kuleta mageuzi
katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Baba
Mtakatifu Francisko. Huu unapaswa kuwa ni mwanzo mpya baada ya kipindi cha kashfa
iliyoikumba Vatican kwa baadhi ya wafanyakazi wake wasiokuwa waaminifu kuvujisha nyaraka
za siri kutoka Vatican kwa mafao yao binafsi. Ni muda wa kujikita zaidi na zaidi katika
uhusiano wa kidplomasia katika kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu; haki
na amani pamoja na mafao ya wengi.
Ni maneno ya Kardinali mteule Pietro Parolin,
Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Gazeti la "Avvenire" linalomilikiwa
na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Changamoto kubwa iliyoko mbele ya Kanisa kwa
sasa ni toba na wongofu wa ndani; upendo na mshikamano wa dhati unaosimikwa katika
msingi wa kanuni auni kwa ajili ya kudumisha mshikamano wa kidugu kati ya watu, kwa
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
mwa Jamii.
Kutokana na changamoto hii anasema Kardinali mteule Parolin, kuna
haja kwa Sekretarieti ya Vatican kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa
la kiulimwengu kwa kuondokana na urasimu usiokuwa na tija wala mashiko; kwa kujikita
katika huduma kwa Kanisa katika ujenzi na uimarishaji wa umoja na utume wa Kanisa
sehemu mbali mbali za dunia. Hiki kinapaswa kuwa ni chombo cha kumsaidia Baba Mtakatifu
na Maaskofu mahalia katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yao.
Mabadiliko
ya miundo mbinu ndani ya Vatican hayana budi kusindikizwa na toba pamoja na wongofu
wa ndani. Licha ya mapungufu ya kibinadamu yanayoweza kujionesha katika Sekretarieti
ya Vatican, lakini bado kuna umati mkubwa wa watakatifu wanaojitoa bila ya kujibakiza
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Baba Mtakatifu anaendelea
kuwahimiza wafanyakazi wa Vatican kutekeleza wajibu wao kama binadamu, wakionesha
upendo na ukarimu pamoja na kushiriki katika dhamana ya utangazaji wa Habari Njema
ya Wokovu.
Wizi wa nyaraka za siri kutoka Vatican ni kati ya mambo ambayo yamemsikitisha
na kumhuzunisha sana Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika maisha na utume wake
kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ni kashfa ambayo imewachafulia watu wengi sifa
zao njema, changamoto kwa wahusika wakuu kuendelea kujiuliza ukweli na uaminifu wao
kwa Injili ya Kristo.
Kardinali mteule Parolin anasema, Benki ya Vatican bado
ina umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa; jambo la msingi ni kuhakikisha
kwamba, inatekeleza dhamana yake kwa kuzingatia misingi ya Injili, maadili, ukweli
na uwazi. Kanisa litaendelea kuwa mstari wa mbele katika kulinda na kutetea misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya mataifa na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa
ina kiu ya amani ya kudumu huko Syria na sehemu nyingine ambako mtutu wa bunduki bado
unaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.
Vatican itaendelea
kujenga na kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na China kwa njia ya majadiliano
katika ukweli na uwazi na wanasiasa nchini humo. Mwelekeo wa Baba Mtakatifu Francisko
katika masuala ya uchumi na maendeleo unajikita zaidi katika misingi ya maadili; upendo
na mshikamano wa kidugu katika kupambana na baa la umaskini, njaa na maradhi sehemu
mbali mbali za dunia, kwa watu kujali na kuguswa na mahangaiko ya jirani zao. Hii
inatokana na ukweli kwamba, pengo kati ya maskini na matajiri linaendelea kuongezeka
maradufu. Vatican itaendelea kushirikiana na Makanisa mahalia pamoja na wadau mbali
mbali kwa ajili ya kutafuta mafao ya wengi.