2014-02-08 10:25:23

Mchakato wa Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, na Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland


Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linamwalika Baba Mtakatifu Francisko kushiriki pamoja nao kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani wakati wa Maadhimisho ya Jubilee ya Miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, itakayofanyika kunako Mwaka 2016 sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.

Mwaliko kwa Baba Mtakatifu umetolewa na Askofu mkuu Jozef Michalik, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, wakati wa kuhitimisha hija ya kitume ya Maaskofu kutoka Poland inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican, mwishoni mwa Juma.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland limeelezea kuhusu utume na maisha ya Kanisa Katoliki nchini Poland linaloundwa na Majimbo 44 na kwamba, asilimia 93% ya wananchi wa Poland wapatao millioni 38 wanajitambua kwamba ni Wakristo kwa vile wamebatizwa!

Maaskofu Katoliki Poland wameshikamana kwa dhati katika mafundisho ya imani, maadili na utu wema; nidhamu na mikakati ya shughuli za kichungaji. Kanisa linaendelea kusimama kidete katika malezi na majiundo endelevu ya Makleri nchini Poland sanjari na utoaji wa huduma makini katika sekta ya elimu na afya. Bado waamini wana imani thabiti na wanahudhuria Ibada na Liturujia mbali mbali za Kanisa na kwamba, asilimia 75% ya wananchi wa Poland wanapinga sera za utoaji mimba.

Mapadre 2, 015 kutoka Poland wanatekeleza shughuli za Kimissionari sehemu mbali mbali za dunia kama Mapadre wa Zawadi ya Roho Mtakatifu, jambo ambalo linalifanya Kanisa Katoliki Poland kuwa na mwelekeo wa kimissionari katika maisha na utume wake. Makleri na watawa wanaendelea kujikita katika katekesi na elimu ya dini shuleni bila kusahau mchango wa Kanisa katika sekta ya mawasiliano ya Jamii. Kuna Kituo cha Televisheni cha Kanisa Kitaifa na walau kila Jimbo Katoliki nchini Poland lina kituo cha Radio kinachofanya kazi barabara.

Baraza la Maaskofu Katoliki Poland kwa sasa linaendelea kujikita katika Uinjilishaji Mpya kwa kuihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake. Kanisa linaendelea kujivunia mafanikio makubwa yaliyokwisha kupatikana katika utume wa shughuli za kichungaji miongoni mwa vijana. Wameanzisha Mfuko wa Millenia ya tatu ya Ukristo unaosaidia vijana 2, 500 wanaotoka katika familia maskini katika masuala ya elimu. Waamini wana moyo na ari ya kufanya hija za maisha ya kiroho ndani na nje ya Poland. Kimsingi waamini wa Kanisa Katoliki nchini Poland wana imani hai inayotolewa ushuhuda katika maisha na vipaumbele vyao.







All the contents on this site are copyrighted ©.