2014-02-07 08:33:23

Watakaoendekeza vitendo vya ukeketaji kukiona cha mtema kuni!


Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Bi Anjela Kairuki amesema Serikali ya Tanzania haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria pamoja na kuwawajibisha ipasavyo maafisa wa serikali watakaothibitika kuwa wanachangia kwa njia moja au nyingine kuendelezwa kwa ukatili wa kijinsia.

Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo kwenye hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na mkuu wa wilaya ya Singida, Bi Queen Mlozi kwenye maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya kupinga vitendo vya ukeketaji duniani (Zero Tolerance to FGM/C Day) iliyofanyika kitaifa katika Kijiji cha Ngimu,tarafa ya Mgori, Mkoani Singida, tarehe 6 Februari 2014.

Aidha Bi Kairuki amesema kuwa ili haki iweze kutendeka kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia Jeshi la Polisi halina budi kuharakisha zoezi la kuanzisha na kuendesha madawati ya jinsia katika wilaya zote na ikiwezekana katika vituo vyote,ili haki iweze kutendeka kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuagiza maafisa wa serikali watakaothibitika kuwa wanachangia kwa njia moja au nyingine kuendelezwa kwa ukatili wa kijinsia kuwa wachukuliwe hatua kali za kisheria na wawajibishwe ipasavyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Programu ya Wanawake,Watoto na Jinsia – CCT,Bi Mary Shuma amesema Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) imeanzisha program ya wasaidizi wa kisheria (Yaani Paralegal unit iitwayo NGIPACE), kwa ajili ya kuwapatia wananchi msaada wa kisheria. Kwa mujibu wa Bi Shuma viongozi wa program hiyo wamejengewa uwezo wa masuala mbalimbali ya kisheria ili waweze kutoa msaada unaostahili.

Naye Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la kiserikali la AFNET, Bi Sara Mwaga akiwasilisha risala ya wanaharakati wa maadhimisho hayo amebainisha kwamba kiwango cha ukeketaji ni kimepungua kutoka asilimia 18 kilichokuwepo awali hadi asilimia 15 ambacho ni pungufu ya asilimia tatu tu.

Kwa mujibu wa Bi Mwaga hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuongeza juhudi za kupinga ukeketaji na umuhimu wa wadau mbali mbali kulipa kipaumbele suala la ukeketaji. Maadhimisho ya siku ya kupinga vitendo vya ukeketaji wa wanawake duniani yaliyoambatana na ujumbe usemao Ukeketaji haukubaliki, yameratibiwa na Kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC), AFNET, DIAC, CCT, WOWAP, TAMWA, TAWLA,World Vision,BAKWATA,CDF,WILAC pamoja na NAFGEM yalifanyika kitaifa Kijiji cha Ngimu,tarafa ya Mgori,Mkoani Singida, nchini Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.