Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya tano ya Kipindi cha Mwaka wa A wa Kanisa
Tunaendelea na kipindi chetu tafakari Neno la Mungu masomo Dominika ya V ya mwaka
A. Masomo yanatualika kuwa chumvi na mwanga wa dunia. Katika somo la kwanza, Nabii
Isaya anatualika kuwalisha na kuwavika maskini. Katika kutenda
kazi hiyo tunakumbuka Heri walio maskini wa roho maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Kwa njia ya Nabii Isaya, Bwana anatangaza matokeo ya kazi njema hiyo, akisema nuru
itakuzukia kama asubuhi na afya yako itakuwa njema na haki daima itakutangulia. Nabii
Isaya haishii katika hayo bali pia anatangaza kuwa sala ya mwenye kutenda huduma kwa
walio maskini itasikikika daima na hapa ndipo kuna furaha timilifu katika mapenzi
yake Mwenyezi Mungu.
Uaguzi wa Nabii Isaya unakuja wakati Waisrael wametoka
utumwani Babilonia katika karne ya 5KK. Katika kipindi hicho, Waisraeli walitarajia
kuwa mateso yangekuwa yamekwisha, lakini badala yake yaliendelea. Basi kwa kuwa katika
nyakati za kale kama kulitokea shida fulani watu walifunga, ni katika mlengo huo basi,
Waisraeli walifunga na kusali ili maisha yao yaweze kukaa sawasawa. Pamoja na jambo
jema hilo la kufunga shida iliendelea yaani matajiri waliendelea kuwanyonya maskini.
Ni katika madhulumu haya Waisraeli walianza kumlalamikia Mungu, kwa nini mambo
hayabadiliki na hivi wakaanza kusema haina haja ya kufunga! Hapa ndipo sasa Nabii
Isaya anakuja na jibu akisema Mungu hana kosa lolote, isipokuwa sala na kufunga kwenu
hakufikii kiwango cha kumpendeza Mungu. Mungu anataka sala na kufunga kuliko na mzizi
katika huduma kwa maskini na wenye taabu mbalimbali katika jumuiya yenu. Mpendwa sala
yako ikoje?
Katika Somo la Pili Mt. Paulo anazidi kutangaza nguvu ya Mungu
ambayo huongoza wahubiri wa Neno lake. Ndiyo kusema hakuna mhubiri anayeweza kujitapa
yakwamba anatangaza injili kwa nguvu zake mwenyewe. Anawaalika Wakorinto watambue
kuwa Neno na ujumbe wa Mungu haulali katika ufasaha na hekima ya kibinadamu kama watu
wenye hekima katika kizazi hicho cha Wakorinto bali ni nguvu ya Msalaba wa Kristo
mfufuka. Yeye mwenyewe anakiri kuwa hakuja kuonesha hekima yake bali kumjua Kristu
tu na ndiyo shime yake. Ndiyo kusema anakiri udhaifu wake ambao utamruhusu aombe msaada
toka kwa Mungu.
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 20:9 inaonekana Mt. Paulo
alipokuwa anahubiri kuna baadhi walianza hata kusinzia na kijana mmojawapo alianguka
kupitia dirishani toka gorofa ya tatu! Ataka kusema nini? Ataka kusema ufasaha hauna
nguvu bali Mungu mwenyewe katika Roho Mtakatifu. Na kama ingekuwa ufasaha ni wa maana,
basi kijana huyu asingeingia katika shida ya usingizi. Hili halikumtisha Mt. Paulo
bali Injili iliendelea kuhubiriwa na kuenea katika Ukorinto yote. Mpendwa unayenisikiliza
Neno lenyewe lina nguvu bila madoido yetu, yafaa kuwa na imani thabiti.
Katika
Injili ya Matayo, ujumbe na mwaliko ni ”kuweni chumvi na nuru”, na kwa namna hiyo
kuangaza mbele ya watu na watu wayaone matendo yenu na wamtukuze Mungu. Mwinjili anatumia
mfano wa chumvi na nuru, ambazo ni alama tumika katika nyakati za kale. Chumvi humaanisha
mambo kadhaa: chumvi huleta radha kwenye chakula na hivi toka zamani ilimaanisha hekima
na busara. Hata hivi leo utasikia watu wakisema, jamaa ana chumvi katika kichwa chake,
wakimaanisha ana hekima na busara katika utendaji wake. Ndiyo kusema Wafuasi wa Kristo
lazima watoe maneno yaliyo ya maana yaani yaliyojaa hekima ya kimungu na si bulaabulaa!
Jaribu kufikiri kama Neno la Mungu lisingekuwa Neno la furaha wapi tungepata
matumaini! Wapi tungepata kutambua kuvumilia taabu na madhulumu katika maisha yetu!
Wakristo ni lazima watoe radha ya kikristo ili maisha ya watu yawe ni maisha ya furaha
na matumaini.
Mpendwa msikilizaji, chumvi si tu radha bali pia hutumika kutunza
vyakula vizioze! Wakristo kwa maana hiyo lazima wawe watunzaji wa maisha ya watu katika
ulimwengu huu. Uwepo wa Wakristu katika ulimwengu ni msaada ili mwanadamu asianguke
katika unyanganyi na ufisadi na hivi dunia ikaangukia katika kuongozwa na misingi
ya shetani.
Mpendwa msikilizaji, kwa kawaida chumvi haipotezi radha yake, sasa
iweje Bwana aseme chumvi iliyoharibika? Bwana katika hili ataka kutuambia kuwa kama
mhubiri anaacha kumtegemea Mungu na hivi anaweka mambo yake mbele basi ile hali ya
Injili uchafuliwa ingawa Injili yenyewe hubaki, lakini kuna uozo huo ambao huchelewesha
kasi yake. Mpendwa mwana tafakari Bwana anatumia mfano wa mwanga akitaka waamini
wawe mwanga unaoangaza wengine ili waweze kuona. Kama ambavyo jua huangaza ili tuone
vema basi nasi vivyohivyo kwa wengine. Mwanga unao wajibu wa kuangaza kumbe hatuweki
macho yetu kwenye mwanga bali kwa kile chema kinachotendwa na mwanga.
Wakristo
si mwanga bali wanategemewa kutenda yaliyomema yaani matendo ya mwanga. Wakristo kwa
vyovyote vile lazima wabaki wamejificha, kwa sababu ukitazama jua moja kwa moja utaharibu
macho, kumbe tunachotakiwa kuona ni hospitali, vituo vya watoto yatima, shule na mambo
yote mema yaani matendo ya mwanga. Mpendwa ni kwa njia ya matendo haya Injili ya Bwana
inasonga mbele kwa kasi mpaka miisho yote ya dunia. Nikutakie furaha na matumaini
katika kuwa mwanga na chumvi ya dunia. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa
kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.