2014-02-07 11:01:45

Mwaka wa Familia Jimbo Katoliki Machakos


Wanandoa wanapaswa kuheshimiana, kuthaminiana na kutunziana uaminifu wa viapo vyao vya ndoa, ili kuhakikisha kwamba, daima ile divai ya upendo, uaminifu, ukarimu, msamaha na udumifu vinatunzwa na kuendelezwa katika maisha ya ndoa na familia.

Uaminifu miongoni mwa wanandoa ni tunu msingi katika kukuza na kudumisha malezi ya watoto ambao ni tumaini la Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Familia zikitekeleza wajibu wake msingi, Kanisa litaweza kuimarika na kuzaa matunda ya wongofu na utakatifu wa maisha kwa watoto wake! Wanandoa wanapaswa kuondokana pia na tabia ya kuvunjika kwa ndoa hata katika uchanga wake hasa kutokana na ukosefu wa uaminifu katika maisha ya ndoa na familia.

Hapa kinachoonekana ni upendo wa vitu na mali, mambo ya mpito! Wanandoa wajenge upendo wa dhati kabisa unaobubujika kutoka katika sakafu ya mioyo yao kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Nyumbani. Maisha yao yawe ni utenzi wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu na harufu nzuri ya matumaini kwa wana ndoa watarajiwa, ili kwa kuona mifano na ushuhuda amini wa watu wa ndoa, vijana wengi wavutwe kufunga ndoa za Kikristo; ndoa zinazopaswa kudumu hadi kifo kitakapowatenganisha!

Hii ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu Martin Kivuva wa Jimbo Katoliki Machakos, Kenya wakati wa Ibada ya Misa Takatifu ya kutoa Daraja Takatifu la Upadre kwa Mashemasi thelathini, kielelezo cha upendo na ukarimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu unaobubujika kutoka katika Familia za Kikristo. Hawa ni vijana ambao wanataka kujitosa kimasomaso kuwatangazia watu Injili ya Furaha kwa njia ya maisha na utume wa Kipadre. Ibada hii ya Misa Takatifu ilikuwa ni sehemu ya Kufunga Mwaka wa Imani uliokuwa umezinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI na kufungwa rasmi na Papa Francisko kwa kishindo kikuu!

Vijana wamechangamotishwa kuwaheshimu, kuwapenda na kuwahudumia wazazi wao kwani wazazi hawana mbadala duniani! Waamini katika ujumla wao wamehimizwa kuendeleza hija ya maisha ya kiroho, matunda na neema walizokirimiwa wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Katika kipindi cha Miaka kumi iliyopita, Jimbo Katoliki la Machakos limefanikiwa kupata maendeleo makubwa katika mikakati yake ya shughuli za kichungaji, jambo la msingi kwa sasa ni kujenga, kuimarisha na kuishuhudia imani yao katika matendo. Waamini wametakiwa kuwasaidia Mapadre wapya kuishi maisha yao ya Kipadre kwa uaminifu, uadilifu, uchaji na majitoleo kamili, kama sehemu yao ya kushiriki mchakato wa kuwatakatifuza watu wa Mungu bila kumezwa na malimwengu.

Askofu Martin Kivuva ametumia fursa hii kuzindua pia Mwaka 2014 kuwa ni Mwaka wa Familia Jimbo Katoliki la Machakos. Ibada hii pia ilikuwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Machakos baada ya Askofu Urbanus Kioko aliyelitumikia Jimbo Katoliki Machakos kwa miaka 29 kung'atuka kutoka madarakani.

Askofu Martin Kivuva tangu alipoteuliwa kuiongoza Familia ya Mungu Jimbmo Katoliki Machakos, kumekuwepo na maendeleo makubwa: kiroho na kimwili. Idadi ya Parokia zimeongezeka kutoka Parokia 42 hadi kufikia Parokia 72 kwa sasa. Jimbo linaendelea kushirikiana na majimbo mbali mbali kutoka Marekani, Ujerumani na Italia katika kuwatangazia watu Injili ya Furaha.







All the contents on this site are copyrighted ©.