Majadiliano ya kidini yanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kujenga misingi ya
haki, amani na utulivu katika Jamii
Baraza la Maaskofu Katoliki India linaendelea na mkutano wake wa thelathini na moja
wa kawaida uliofunguliwa hapo tarehe 5 Februari na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe
12 Februari 2014. Askofu mkuu Salvatore Pennacchio, Balozi wa Vatican nchini India
amelitaka Kanisa kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa majadiliano ya kidini
nchini India pamoja na kuhakikisha kwamba, waamini wanapata huduma makini za kichungaji
kutoka kwa Maaskofu wao mahalia.
Kama sehemu ya Unjilishaji Mpya Kanisa halina
budi kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kuimarisha misingi
ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa watu wa dini na imani
mbali mbali nchini India. Katika mikakati yake ya kichungaji, Kanisa linapaswa kwanza
kabisa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa
Jamii, ili wao pia waweze kuonja na kufarijika kwa Injili ya Furaha inayomwilishwa
katika imani tendaji.
Kanisa bado linahamasishwa kuendelea kujichotea utajiri
unaofumbatwa katika Mafundisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na
utume wake! Mkutano huu unahudhuriwa na Maaskofu 200 kutoka katika Majimbo 167 yanayounda
Kanisa Katoliki nchini India. Maaskofu pamoja na mambo mengine wanajadili kuhusu uchaguzi
mkuu nchini India unaotarajiwa kufanyika kati ya Mwezi Aprili na Juni 2014.