Vatican itatekeleza maoni yaliyotolewa, lakini haitakubali kuingiliwa katika Mafundisho
tanzu ya Kanisa!
Baada ya kumalizika kwa mkutano wa sitini na tano wa kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu
Haki za Mtoto na kutoa maoni yake baada ya kujadili kwa kina na mapana taarifa iliyowasilishwa
kwenye mkutano huu na ujumbe wa Vatican pamoja na nchi nyingine wanachama yaani Congo,
Ujerumani, Ureno, Russia na Yemen.
Kadiri ya mchakato ulioainishwa kwenye
mkataba wa Haki za Mtoto, Vatican itaendelea kuyafanyia kazi maoni yaliyotolewa kuhusu
taarifa yake kwa kuheshimu haki na utekelezaji wake kimataifa bila kusahau mchango
wa Vatican wakati wa mkutano huo uliofanyika hapo tarehe 16 Januari 2014.
Vatican
inasikitika kuona kwamba, baadhi ya maoni yaliyotolewa na kamati hii yana mwelekeo
wa kutaka kuingilia na kuvuruga Mafundisho Tanzu ya Kanisa Katoliki kuhusu utu na
heshima ya binadamu pamoja na utekelezaji wake wa uhuru wa kidini. Vatican inaendelea
kujikita katika kulinda na kutetea haki msingi za watoto mintarafu kanuni na njia
zilizoainishwa kwenye Mkataba wa Haki za Mtoto pamoja na kuzingatia tunu msingi za
maisha ya kimaadili na kiroho zinazofundishwa na Kanisa Katoliki.