2014-02-06 09:54:14

Mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu unaweza sasa kupatikana kwenye tovuti!


Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki limezindua tovuti yake inayotoa habari muhimu kuhusu mchango wa Kanisa Katoliki katika sekta ya elimu ya juu, sehemu mbali mbali duniani. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Itifaki iliyoridhiwa kati ya Vatican na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika masuala ya sekta ya elimu kimataifa kwa kutambua na kuthamini vyeti mbali mbali vinavyotolewa na Vyuo vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zinazoongozwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki.

Hii ni fursa kwa Vatican kuendelea kuchangia kwa kina na mapana katika sekta ya elimu kwa kutoa habari zinazoonesha mchango wa Kanisa ili kushirikishana na nchi nyingine ambazo tayari zimekwisharidhia Itifaki hii pamoja na UNESCO. Tovuti ya Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwa sasa lina sehemu kuu mbili: Sehemu ya kwanza inazungumzia Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki na majukumu yake kwa ujumla.

Sehemu ya pili imesheheni hati na nyaraka mbali mbali zinazoweza kufanyiwa rejea na wasomi kuhusu: Hekima ya Kikristo na Hati ya Kanisa kuhusu Vyuo Vikuu vya Kikatoliki. Tovuti hii inaonesha uhusiano wa kimataifa kati ya Baraza la Kipapa la Taasisi mbali mbali katika sekta ya elimu. Watumiaji wa tovuti hii wanaweza pia kupata takwimu na habari kutoka katika "Pango hifadhi ya Nyaraka za Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki". Ukitaka kufaidi zaidi unaweza kutembelea Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki kwa anuani ifuatayo: www.educatio.va








All the contents on this site are copyrighted ©.