Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu wanayo dhamana ya kujenga na kukuza
majadiliano ili kudumisha haki, amani na upendo kati ya watu!
Chuo Kikuu cha Notre Dame chenye tawi lake mjini Roma, hivi karibuni kiliwatunukia
Udaktari wa heshima Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano
ya Kidini pamoja na Mama Maria Voce, Rais wa Chama cha Kitume cha Wafokolari kutokana
na mchango wao makini katika kudumisha majadiliano ya kidini miongoni mwa watu wa
Jumuiya ya Kimataifa.
Hili lilikuwa ni tukio la furaha na heshima kubwa kwa
Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Notre Dame kumtunukia pia udaktari wa heshima Padre John
Jenkins, CSC, Rais wa Chuo Kikuu cha Notre Dame kutokana na mchango wake katika sekta
ya elimu. Watunukiwa wote walizungumzia kuhusu mchango wa Vyuo Vikuu vya Kikatoliki
pamoja na Taasisi za Elimu ya Juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki
sehemu mbali mbali za dunia, katika kujenga na kudumisha majadiliano ya kitamaduni,
kiimani na kiakili.
Wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu daima
wako kwenye mchakato wa majadiliano ya kidini, unaopania kujenga na kudumisha haki,
amani, upendo na mshikamano wa dhati kati ya watu wa mataifa anasema Kardinali Jean
Louis Tauran.
Kwa upande wake, Mama Maria Voce, Rais wa Shirika la kitume la
Wafokolari amekazia umuhimu wa Jumuiya za Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu kujikita
katika fadhila ya upendo na maisha; mambo msingi yanayobubujika kutoka katika tunu
msingi za Kiinjili.
Tafakari ya kina ya Neno la Mungu inaweza kuwajengea wanafunzi
uwezo wa kufahamu na kuimwilisha sheria ya upendo kwa Mungu na binadamu katika kudumisha
mahusiano mema kati ya watu. Ni katika Injili ya Upendo kwa Mungu na Jirani, watu
wanaweza kugundua ile furaha ya kuwa ni wadau katika ujenzi wa ulimwengu unaosimikwa
katika misingi ya haki, upendo, amani na udugu.
Chuo Kikuu cha Notre Dame tawi
la Roma linatoa huduma ya elimu kwa wale wanaotaka kujiendeleza zaidi kwa kupata fursa
ya masomo nje ya Italia. Ni mahali pa kukuza na kuendeleza shughuli za elimu na utamaduni
kutoka mjini Roma.