2014-02-05 11:16:29

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inaadhimisha Miaka 46 tangu ilipoanzishwa!


Zaidi ya Maaskofu mia moja kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanahudhuria mkutano wa kila Mwaka unaoandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake makuu mjini Roma. Maaskofu kwa mwaka huu wanatafakari kuhusu Injili ya Furaha, Waraka wa Kitume uliochapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wanaangalia mbinu na mikakati inayoweza kutumika katika utangazaji wa Injili ya Furaha kwa kuzingatia kwamba, Mama Kanisa kwa sasa anajielekeza zaidi katika shughuli za Kimissionari zinazojikita katika ushuhuda makini wa Injili ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo ya kidugu.

Siku ya Alhamisi, tarehe 6 Februari 2014 majira ya saa 12: 30 kwa saa za Ulaya, Askofu mkuu Giovanni Angelo Becciu, Katibu mkuu mwambata wa shughuli za kiutawala katika mji wa Vatican anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 46 tangu Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilipoanzishwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.