Ndoa na Familia ni kati ya vipaumbele vya kichungaji vya Askofu mkuu Ramaroson!
Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na majiundo makini ni kati ya vipaumbele
vya kichungaji vinavyofanyiwa kazi na Askofu mkuu Benjamin Marc Ramaroson wa Jimbo
kuu la Antsiranana, nchini Madagascar. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Ramaroson aliteuliwa
hivi karibuni kuwa Askofu mkuu na Baba Mtakatifu Francisko na kusimikwa rasmi hapo
tarehe 25 Januari 2014, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Siku kuu ya Kuongoka kwa
Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa.
Anasema, kati ya vipaumbele vyake
vya kwanza ni majiundo makini ya tunu msingi za maisha ya ndoa na familia pamoja na
kutoa majiundo endelevu kwa vijana ili waweze kutambua dhamana na nafasi yao katika
maisha na utume wa Kanisa, tayari kumshuhudia Kristo na Kanisa lake kwa watu wanaokutana
nao katika medani mbali mbali za maisha na kwa njia hii, wawe tayari kushuhudia Injili
ya Furaha. Familia na Vijana ni kati ya makundi yanayoathirika vibaya kutokana na
kinzani mbali mbali za kisiasa na kijamii nchini Madagascar.
Kumong'onyoka
kwa tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili ni changamoto kubwa kwa Wakristo na
watu wenye mapenzi mema katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na
teknolojia. Kuna haja kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, wanayatakatifuza malimwengu
kwa njia ya utakatifu wa maisha yanayobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili;
ili watu waonje Injili ya Furaha inayoendelea kutangazwa na Wakristo katika Mapambazuko
ya Millenia ya tatu ya Ukristo.
Waamini waendelee kutumia vyema karama na
neema walizokirimiwa wakati wa Ubatizo na Kipaimara; waoneshe ari, mwamko wa kimissionari
na huduma ya mapendo kwa jirani kama kielelezo cha imani katika matendo! Hii ni changamoto
endelevu katika maisha na utume wa waamini hata baada ya kuhitimisha Maadhimisho ya
Mwaka wa Imani.
Madagascar kwa sasa inahitaji kuanzisha mchakato wa maendeleo
endelevu yanayojikita katika elimu makini kuhusu haki na amani; upatanisho na upendo
kwa Mungu na jirani hasa kufuatia kinzani na migogoro ya kisiasa iliyojitokeza nchini
humo kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa demokrasia miongoni mwa wananchi.