Kuna ukata wa rasilimali fedha ili kukabiliana na uhaba wa chakula duniani!
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP limelazimika kupunguza mikakati yake ya
kusaidia maeneo yanayokabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na ukosefu wa rasilimali
fedha. Shirika hili linahitaji zaidi ya dolla za Kimarekani billioni moja katika kipindi
cha mwaka 2014 ili kukabiliana na uhaba wa chakula unaoendelea kujitokeza katika nchi
kadhaa duniani.
Hayo yamebainishwa na Bi Erthrin Cousin, mkurugenzi wa Shirika
la Mpango wa Chakula Duniani wakati wa ziara yake ya kikazi katika nchi wafadhili
ili kuzihamasisha kuchangia zaidi. WFP inalazimika kutumia kiasi cha dolla za Marekani
40, 000 kwa juma kwa ajili ya kuwahudumia wananchi millioni nne waliokimbia makazi
yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao nchini Syria. Hali bado ni tete huko Haiti,
Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Zimbabwe, DRC, Madagascar, Niger, Mali na Kenya.
WFP
inapenda kuhamasisha wadau mbali mbali kuchangia kwa kuwashirikisha pia watu, mashirika
na makampuni ya watu binafsi kama ambavyo UNICEF inavyofanya kwa ajili ya kugharimia
miradi mbali mbali ya huduma kwa watoto wadogo sehemu mbali mbali za dunia.
Ni
matumaini ya WFP kwamba, nchi nyingine zitaendelea kuiga mfano wa China na Falme za
Kiarabu katika kuchangia fedha ili kukabiliana na ukosefu wa chakula sehemu mbali
mbali za dunia. Wafadhali wa kawaida wanaendelea kuhamasishwa kuchangia mara kwa mara
kwani WFP inawategemea sana.