Hotuba ya DR. Jakaya Mrisho Kikwete Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati
wa sherehe ya kuadhimisha siku ya sheria nchini tarehe 3 Februari, 2014 Dar es Salaam. Mheshimiwa
Jaji Mkuu; Nakushukuru sana Mheshimiwa Jaji Mkuu kwa kunialika kwa mara nyingine
tena kuja kujumuika nanyi kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria Nchini na ya Mahakama
kuanza kazi mwaka huu. Ni jambo la busara kuwa siku hii inaadhimishwa kila mwaka.
Inatupa fursa nzuri sisi tusio wanasheria kujifunza masuala mengi yahusuyo sheria
na utoaji haki nchini.
Naomba na mimi niungane na wenzangu walionitangulia
kukupongeza na kukushukuru Mheshimiwa Jaji Mkuu, Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na watumishi
wote wa Mahakama kwa kazi nzuri mliyofanya mwaka jana. Nami nawatakia mafanikio mema
na utendaji mzuri zaidi katika mwaka huu wa 2014.
Kaulimbiu ya Mwaka Huu
Mheshimiwa
Jaji Mkuu; Kama ilivyo kawaida yenu, kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema
“Utendaji haki kwa wakati: Umuhimu wa Ushiriki wa Wadau” imebeba ujumbe mzito na muhimu
kwa wadau wa utoaji haki nchini. Kwa jumla inatukumbusha kuwa ili haki iwe na maana,
ni lazima ipatikane kwa wakati. Msemo wenu maarufu wa “Justice delayed is justice
denied” unaelezea kwa ufasaha dhana hii. Ni ukweli usiopingika kwamba ili haki ipatikane
kwa wakati, ushiriki kwa ukamilifu wa wadau wote ni jambo la lazima. Wadau hao ni
pamoja na Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, Polisi, TAKUKURU, Mawakili, Serikali
na wengineo.
Endapo mmoja wa wadau hao atashindwa kutimiza wajibu wake ipasavyo,
haki ya mtu au watu itachelewa kupatikana au itadhulumiwa. Hali hii inatokana na
ule ukweli kwamba kila mdau anao wajibu maalum ambao hana budi kuutimiza. Ufanisi
wa mmoja unategemea sana utendaji wa mwingine. Ni kama mwili wa binadamu ulivyo,
kila kiungo kina nafasi yake, kimoja kisipofanya kazi vizuri siha ya mwili hodhoofika.
Ndiyo hivyo ilivyo pia kwa mfumo wa utoaji haki.
Mahakama ambapo ni kilele
katika mtandao au mfumo wa utoaji haki haikamati wahalifu, haipelelezi mazingira ya
utendaji kosa, haitayarishi wala haiendeshi mashtaka. Hivyo basi, kazi ya Polisi,
TAKUKURU na Mkurugenzi wa Mashtaka husaidia sana kuharakisha utoaji haki, Mahakama
ina uharaka wa kusikiliza kesi hasa pale ambapo upelelezi umekamilika mapema na waendesha
mashtaka wako tayari, na pia, uharaka wa upatikanaji wa nakala ya hukumu ili mtu
aweze kukata rufaa kwa wakati.
Mheshimiwa Jaji Mkuu;
Masuala
mengi kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu umeyaeleza vizuri pamoja na wazungumzaji waliotangulia.
Jambo kubwa na muhimu ambalo limejitokeza ni kuwa ushiriki na ushirikiano wa wadau
ni muhimu sana katika utoaji haki kwa wakati. Mahakama ni kilele katika mfumo wa
utoaji haki nchini. Lakini, Mahakama haipelelezi, haifikishi wahalifu mahakamani,
haiendeshi mashtaka. Hasikilizi mashauri na hutoa kutoa uamuzi kuhusu upande upi
una haki.
Hivyo, wale wapelelezi na waendesha mashtaka na wanaotetea wasipofanya
kazi yao ipasavyo haki huchelewa. Hii ina maana kuwa Polisi wahakikishe wahalifu
wanakamatwa, upelelezi unafanyika kwa makini na kesi zao zinapelekwa kwa Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka ili zipelekwe Mahakamani.
Hivyo kwa TAKUKURU nao wahakikishe
kuwa upelelezi unafanywa vizuri ili shauri linapofikishwa Mahakamani halichelewi kwa
sababu ya upelelezi kutokukamilika. Mkurugenzi wa Mashtaka nae ahakikishe shauri
analolipeleka limeandaliwa vizuri ili lichukue muda mfupi kusikilizwa na kuamuliwa.
Weledi na uadilifu wa Polisi, TAKUKURU na DPP ni mambo ya msingi sana. Hivyo hivyo,
Mawakili nao wana nafasi yao. Naambiwa kuna wakati shauri huaihirishwa kwa sababu
ya wakili wa utetezi kushindwa kufika Mahakamani. Ukiacha sababu ya kuumwa lakini
wakati mwingine ni kwa sababu ya kuwa na kesi mahali pengine.
Nafasi
ya Mahakama
Mheshimiwa Jaji Mkuu; Ni ukweli usiopingika kuwa Mahakama
inayo nafasi ya pekee katika mfumo wa kutoa haki nchini. Nakubaliana na wale wanaouita
Mhimili huu wa dola kuwa ni “The temple of Justice” kutokana na ukweli kwamba watu
wanapokuja Mahakamani wanategemea kutendewa haki. Hakuna mahali pengine pa kukimbilia
kutafuta haki zaidi ya Mahakamani. Wanaweza wasijue sheria za vitabuni, lakini wakajua
haki yao. Hivyo, Waheshimiwa Majaji, Mahakimu na watumishi wengine wa Mahakama mnayo
dhamana na wajibu mkubwa wa kusimamia sheria kwa haki. Ili haki itolewe bila upendeleo
wa aina yoyote ile.
Matarajio ya wananchi ni kuwa kesi zisicheleweshwe kusikilizwa
na kuamuliwa. Pale ambapo upelelezi umekamilika na mashtaka yametayarishwa vizuri
kuahirishwa kusikilizwa kwa kesi huzaa manung’uniko. Pale shauri linapoamuliwa kutolewa
kwa nakala ya hukumu ili anayetaka kukata rufaa afanye hivyo ni jambo la muhimu.
Kinyume chake watu wanakata tamaa na kuamua kuchukua njia za mkato ambazo madhara
yake ni makubwa. Wanakuwa hawana mahali pengine pa kupeleka mashtaka yao. Ndiyo
maana nakubaliana na kauli yako Mheshimiwa Jaji Mkuu kwamba tusiiache misingi ya haki
ikamomonyoka katika jamii yetu mpaka ukafika wakati watu wakaamini kwamba bila kutumia
jambia hakuna haki. Naomba muendelee na kazi nzuri muifanyayo ili muwe kimbilio la
uhakika kwa yeyote ambaye anajiona haki yake inadhulumiwa.
Mheshimiwa Jaji
Mkuu; Nimefarijika sana kusikia kwamba mmejiwekea utaratibu mzuri na misingi ya
ushirikiano wa mawasiliano baina yenu na wadau wengine kwa ajili ya kuboresha utendaji
wenu. Utaratibu huo utasaidia sana kuhakikisha upelelezi wa mashauri unakamilika
haraka na haki inapatikana kwa wakati. Vilevile nawapongeza kwa kuelewa umuhimu wa
kuhuisha sheria, kanuni na taratibu mara kwa mara ili kukidhi mahitaji ya wakati.
Bila shaka hatua zote hizi zitasaidia sana kutatua changamoto ya siku nyingi ya ucheleweshwaji
wa kesi.
Wajibu wa Serikali
Mheshimiwa Jaji Mkuu Napenda kukuhakikisha
kuwa sisi Serikalini tutaendelea kutimiza wajibu wetu ili Mahakama na wadau wengine
wa utoaji haki wafanye kazi ipasavyo. Kwanza tumechukua na
tunaendelea kuchukua hatua kadhaa kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali kufuatia
tafiti na mapendekezo ya Tume zilizoundwa kuangalia mifumo yetu ya kutoa haki kwa
lengo la kuiboresha. Kazi hiyo tunaendelea nayo. Tumeanza na kurekebisha sheria
na mifumo ya utoaji haki na kuweza kutenganisha upelelezi na uendeshaji wa mashtaka.
Pili, tumeanza kuchukua hatua thabiti kuongeza bajeti ya Mahakama ili muweze
kutimiza kwa ufanisi zaidi wajibu wenu. Mwaka huu wa fedha kwa mfano, tumetenga
shilingi bilioni 86 kwenye Mfuko wa Mahakama na shilingi bilioni 42.7 kwa ajili ya
maendeleo. Kiasi hiki ni kikubwa maradufu ukilinganisha na mwaka wa fedha uliopita
ambapo zilitengwa shilingi bilioni 57 kwa shughuli zote. Pamoja na hatua hii muhimu
tumejitahidi sana kuwezesha Mahakama kuongeza rasilimali watu, yaani Majaji Mahakimu
na watumishi wengine. Idadi ya Majaji wa Rufani sasa imefikia 16 kutoka 9 waliokuwepo
mwaka 2005, na wa Mahakama Kuu ni 69 kutoka 35 waliokuwepo mwaka 2005. Nilishakubali
Majaji 20 wapya waajiriwe. Nileteeni mapendekezo niteue. Vilevile idadi ya Mahakimu
imeongezeka zaidi na kufikia 672 na tayari kibali cha kuajiri wengine 300 kimeshapatikana.
Hivi sasa mchakato wa ajira ya wahitimu wa sheria katika Mahakama za Mwanzo unaendelea.
Kufuatia
mapendekezo ya Kamati za Jaji Mrosso na ya Jaji Lubuva, tumekamilisha mchakato wa
kutenganisha shughuli za kutenda haki na utawala kwa kuanzisha nafasi ya Mtendaji
Mkuu. Sasa hivi naambiwa pamekuwa na nafuu sana kwani mzigo waliokuwa nao Majaji
kwenye masuala ya utawala haupo tena. Nasikitika kuwa idhini ya Muundo wa Mahakama
umechelewa kuliko kawaida. Naahidi kuwa litakamilika wiki hii. Tumeendelea kuziongezea
uwezo wa rasilimali fedha, vitendea kazi na nguvu kazi Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
na TAKUKURU.
Mheshimiwa Jaji Mkuu; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
nayo pia imefanyiwa marekebisho makubwa. Shughuli za Wizara zilizokuwa zimechanganyika
na zile za Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali sasa hivi zimetenganishwa. Wizara
imebaki na jukumu lake la kusimamia sera na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu inafanya shughuli
za kisheria. Hatukuishia hapo. Tumefikia hatua nzuri ya kutenganisha shughuli za
upelelezi na za kuendesha mashtaka. Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka imebaki na majukumu
yake ya kusimamia mashtaka na Polisi, TAKUKURU na wengineo wanabaki na majukumu yao
ya ukamataji wa wahalifu na upelelezi. Tunafanya yote haya kuboresha mifumo ya kutoa
haki nchini.
Mwisho
Mheshimiwa Jaji Mkuu; Mabadiliko yaliyofanyika
yana lengo zuri la kuboresha taratibu zetu za kutoa haki nchini. Jambo kubwa ni mabadiliko
kwa jamii na watendaji wenyewe. Watoaji haki ni lazima wajipime kwa matakwa na mahitaji
yao. Endeleeni kutekeleza majukumu yenu mkielewa kwamba wananchi na jamii wanawategemea
katika kuhakikisha kwamba haki inatolewa kwa wakati. Wadau wa utoaji haki muendelee
kutimiza wajibu wenu wa kutatua migogoro, kuwapatanisha wananchi na kuwaadhibu wahalifu
ili amani na utulivu nchini mwetu idumu. Watu wawe na maelewano na waishi bila wasiwasi.
Naomba
kila mmoja wetu ashiriki kikamilifu kuhakikisha lengo letu linafikiwa. Kila mmoja
wetu anayo nafasi yake, hili siyo jukumu la polisi peke yao, Mwanasheria Mkuu au Jaji
Mkuu. Ni jukumu la wote. Basi mwaka huu tujitahidi kufanya vizuri zaidi, kila mtu
afanye hivyo mahali alipo. Bila shaka haki itapatikana kwa wakati. Asanteni sana
kwa kunisikiliza.