Wapeni wanandoa nafasi ya kujinafasi! Msiwawekee kiwingu!
Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, Kipindi cha Kanisa la Nyumbani kilichopita,
tumehekimishana juu ushiriki wa Jamii katika kuifanya ndoa ianze vyema na kustawi.
Tuliangazia
kwanza wajibu wetu wa kuwaombea wanandoa ili waweze kustawi kama mtende wa Lebanoni
na pili, tunatakiwa kuwapatia ushuri mwema, kila mmoja wetu akijitahidi kuwa na ”kifua
kipana”, yaani kubeba na kutunza siri za wanandoa. Leo tunaendelea na sehemu ya tatu!
Tatu,
TUWAPE NAFASI:- Watu wa ndoa, hasa ndoa changa, wanahitaji muda wa kufahamiana zaidi,
kuendelea kukua, kujijenga, kufurahiana wao wenyewe nk. Hapa tutoe mwito pia kwa
baadhi ya ndugu. KUWENI NA MIPAKA, tena iweni na aibu takatifu. Tabia ya ndugu kwenda
kujazana nyumbani kwa waana waliotoka tu kuoana, ni kuwabana mno.
Utashangaa
ukoo mzima wa Bibi harusi wamejaa tele hapo, wameleta matatizo yao yote. Ukoo wa Bwana
harusi wamejaa humo, na ni wakorofi, walafi na wapekuzi ajabu. Mwisho wanaishia kuwachonganisha
wanandoa-changa. Bandika – bandua, akitoka huyu, anakuja huyu. Ndugu wawe na mipaka,
ndoa ya mtoto wenu sio sokoni. Wanahitaji faragha hao.
Nne, KUTAWALA MIDOMO
YETU: Katika hili, mang’amuzi yatatushuhudia kwamba, mara nyingi sana jamii tumechangia
kuyumbisha ndoa za watu kwa kukosa matumizi ya busara ya midomo yetu. Kanuni moja
inatuelekeza hivi: Sio kila unachokijua lazima ikiseme! Vingine kaa navyo kimya tu
- ufe navyo, wala jeneza halitakuwa zito!! Sasa ewe mtu, kuna mambo unayajua kuhusu
mke wa fulani au mume wa fulani.
Usikurupuke tu na kuanza kutangaza au kwenda
kumwambia mama fulani habari-hatarishi unazozijua za mumewe; au unamwambia baba habari
hatarishi za mkewe. Na unapokwenda kumwambia, humwambii habari kama ilivyo, lazima
utatia chumvi nyingi na pilipili yenye kuwasha, ambayo lazima itawachachafya na kutikisa
safari yao ya agano tu; na wakitikisika, wewe unafurahi!! Hapana!! Kama ni lazima
sana, ukiona mama fulani anafanya kinyume – nenda kamwambie yeye mwenyewe, tena umkanye
kabisa.
Sio umamchekea tena na kumsaidia katika uovu, halafu unamzunguaka
na kwenda kumripoti kwa mumewe. Ukiona baba fulani anafanya visivyo; MWAMBIE YEYE
MWENYEWE, UMKANYE, usipitilize tu kwenda kumpelekea BP mkewe. [Kwa habari ya uchongezi
na uchonganishi; soma kwa kutafakari YbS, 28:13 – 26]
Tano na Mwisho: TUTAKIANE
MEMA. Roho mbaya zinazojengeka katika mioyo ya watu, ni sumu kwa usitawi wa ndoa na
Kanisa la Nyumbani. Kuna watu ni waharibifu tu, wanapenda wenzao waharibikiwe. Kama
tulivyokwisha kusema hapo juu, ni wajibu wetu sisi sote kusaidiana katika kulijenga
Kanisa la Nyumbani, hatutatimiza adhma hiyo kama hatutakiani mema.
Tujijengee
dhamiri iliyo njema, yenye kupenda na kufurahia usitawi wa wengine pia. Kama wewe
una roho mbaya, hupendi mafanikio ya wenzako; na wakifanikiwa wewe unaharibu; halafu
wakati huohuo, unamwomba Mungu akusaidie ufanikiwe; unadhani sala yako itapata kibali
kweli? Mwenyewe katika Neno lake ametukataza, usimtendee mwenzako lile usilopenda
kutendewa. Kumtakia mema mwenzako na kumsaidia mwenzako ili kuyapata yaliyo mema,
ni kujibariki mwenyewe na kujifungulia milango ya baraka zaidi.
Katika kipindi
kijacho tutaanzazia mambo ya jumla ambayo yanaweza kuathiri utimilifu wa Agano la
ndoa tangu mwanzoni; YAANI VIZUIZI VYA NDOA, kadiri ya sheria ya Kanisa. Asanteni
kwa kuwa nami, kutoka katika Studio za Radio Vatican, kukuletea kipindi cha Kanisa
la Nyumbani ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.